Soko la wauzaji vyakula la Namtumbo
Soko la Namtumbo kwa ndani
Vitunguu bwelele
Nyanya, Tangawizi bwelele
Maharage na njugu bwelele
Karanga a.k.a Mtesa
Viazi
Jambo,
Ni matumaini yangu kuwa wapiganaji wenzangu tunaendelea na jukumu letu la kuwatumikia watanzania.
Tuendelee kufanya hivyo licha ya changamoto tunazokutana nazo.
Ndugu zangu nimepita katika Soko la mazao na bidhaa ndogondogo la Namtumbo Mjini Mkoani Ruvuma na nikiwa hapo kengele ikagonga
Imegonga baada ya kushuhudia vilio vya wauzaji wa Matunda, mbogamboga na vyakula vingine wakilia ugumu wa biashara. wanadai soko huporomoka sana kipindi hiki cha Mvua kwa kuwa wanunuzi wengi huhamia mashambani wakishughulika na kilimo. Bidhaa nilizoziona sokoni ni pamoja na Nyanya, Vitunguu, viazi, mbogamboga na matunda. Staili inayotumia kuuza bidhaa hizi ni ile ile ya hata kabla Tanzania haijapata uhuru, bidhaa zote zingali zinauzwa zikiwa na thamani ya shambani, hazijaongezwa thamani
Kwa hilo nikakumbuka wajibu wetu waandishi wa habari, kwamba katika safari ya kuongeza thamani bidhaa za wakulima wadau mbalimbali wanapaswa kuhusika, kwanza wadau wa maendeleo matharani taasisi za mitaji, wataalamu wa mashine za kusindikia mazao, wataalamu wa kilimo na usindikaji na wengineo ikiwemo serikali. Sio lengo langu kuwajadili hao
Kengele yangu iligonga kwa swali moja kwamba je sisi waandishi wa habari tumetimiza wajibu wetu wa kuwasaidia wakulima wa Tanzania kuanza na kuchochea safari ya kuongeza thamani ya mazao yao? tumewaonesha fursa zilizopo? tumewaonesha pa kuanzia? Kama tumefanya inatosha? Na kama inatosha tumepima utekelezaji wake na matokeo yake? Na je tunawakumbusha wadau wengine juu ya wajibu huu? kama tumefanya inatosha? Na pia je tumepambana kidete kama tunavyopambana katika masuala ya wanasiasa?
Sio lengo langu kutaka tujilaumu bali kukumbushana kuwa huu ni wajibu mwingine tunaoweza kuwasaidia wakulima. Nafahamu yapo maeneo mengi ya nchi hii yenye shida hii. Naomba tulione hili na tuamue kulivalia njuga. tusipofanya hivi watanzania hasa walala hoi wanaendelea kuumia. Tupige kelele watanzania wale Nyanya za Tanzania popote walipo badala ya baadhi ya watanzania ama watu wanaokuja nchini kwetu kununua nyanya kutoka nje ya nchi. Na sio kwa nyanya tu hata bidha nyingine. Huu ni wakati wa Mvua embe kiasi gani za wakulima zimeoza vijijini kwa kukosa kusindikwa? mbogamboga kiasi gani zinatupwa ama kuachwa ziharibika mashambani?
Tuamue tunaweza kwani sisi ni mhimili wa nne wa Dola japo sio rasmi
Natoa hoja