Sunday, December 29, 2013

Hongera Majjid Mjengwa, Wadau sisi vipi?




Hongera Majjid Mjengwa,

Wiki hii inayomalizika mdau mwenzetu katika tasnia ya habari, mchambuzi mkongwe, mwandishi kindakindaki, mfuatiliaji na mdadavuaji wa habari na matukio na mengine mengi Majjid Mjengwa ameweka sokoni kitabu chake kinachomuelezea gwiji wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na mpigania ukombozi wa Taifa la Afrika ya Kusini, Hayati Mzee Nelson Rolihlahla Mandela.

Mjengwa ameandika kitabu hiki wakati muafaka na amewatendea haki wanajamii hasa wale ambao ama kwa sababu za umri, zama, ama kwa sababu ya kukosa fursa ama kwa sababu nyingine hawakupata kujua kuhusu mwanasiasa huyo Mkongwe alivyojitolea maisha yake kuipigania Afrika ya Kusini iliyokua imetumbukia katika janga la ubaguzi wa rangi ulioendeshwa na makaburu.

Ni sawa Mjengwa ameandika mengi yenye manufaa kwa jamii na ndivyo alivyo kwa tunayefuatilia maisha yake ya uandishi.

Lakini mimi nimeona katika Blog hii Nimpongeze Ndugu Mjengwa kwa sababu alichokifanya ni wajibu wa kila mtu aliyehifadhi historia, taaluma na fursa ya kukiunganisha kizazi cha sasa  na yale yaliyojiri kabla yake.

Katikati ya mwaka 2013 nilihudhuria kongamonano moja lililomwalika Askofu Mstaafu Norbert Mtega katika Jubilei ya kumpongeza Padre Christian Mhagama mmoja wa waandishi wazuri wa vitabu, Askofu Mtega katika Siku hii alisema “Msomi asiyeandika vitabu ni sawa na Mama mjamzito asiyezaa”

Kwa maana hii Mjengwa na waandishi wengine wa vitabu wanatimiza wajibu wao, na wale wasiofanya hivyo wakati wana taaluma ya kufanya hivyo hawatimizi wajibu wao.

Japo kuwa sijapata nakala ya kitabu cha simulizi za Mzee Mandela cha Mjengwa, mimi ni mmoja wa wasomaji wa Blog ya Mjengwa kila uchao na nimefuatilia maandalizi yake kwa kuwa alikua akiweka kwenye Blog yake kila anapofanya tafsiri ya kile kitabu cha Mzee Madiba cha safari ya Ukombozi yaani “Long work to Freedom” Kwa kweli nikiri kuwa hata mimi sijakisoma kitabu hicho cha Madiba na hivyo nilivutiwa mno na simulizi iliyokua ikitafsiriwa na Mjengwa kwenye Blog yake.

Kuna mengi ya kuyasema lakini katika pongezi nimalizie kwa kusema Hongera sana Mjengwa na hongera kwa kuona umuhimu wa kuchapisha kitabu ili iwe kumbukumbu sahihi kwa kila anayetaka kusoma Simulizi za Mzee Mandela na endelea kufanya hivyo kwa mambo mengine mengi yaliyo hazina kwenye kichwa chako kama ilivyo kwaida yako.

Wadau sisi vipi?

Nauliza swali hili kwa sababu naamini kuwa wengi wanaweza kufanya kama alivyofanya Majjid Mjengwa katika simulizi za Mzee Madiba. Hasa kwa sisi waandishi wa habari na katika hili nawagusa zaidi waandishi wa habari wakongwe ambao mimi naamini wana mambo mengi mazuri ya kukisimulia kizazi hiki cha leo hapa Tanzania kuliko watu wengine.

Ndio, wanahabari tunayo fursa hii kwa sababu tunaona mengi. Najiuliza hapa Tanzania Mwalimu Nyerere amefanya mengi katika kupigania uhuru, kuijenga Tanganyika, kuiunganisha Tanganyika na Zanzibar na mengine mengi. Yapo yaliyokua kama vitimbwi, yapo yaliyoonesha uthubutu wa hali ya juu, yapo yaliyoonesha kujitolea hata kufa, yapo yaliyoonesha ujasiri ambao unaonekana leo kama vitu visivyowezekana na mengine kibao.

Haya yote yalifanyika mbele ya waandishi wa habari. Jamani tupeni utamu, tupeni historia, achieni kalamu zenu zitembee, msiache uhondo huo uteketee, msisubiri waje wazungu watafiti ndio waandike.

Akina Mzee Abdul Ngalawa, Ahamed Kipozi, Jenerali Ulimwengu, Phili Karashani, Ernest Mrutu, Agustino Mbunda, Ben Kiko, Hamza Kasongo, Mhidin Michuzi na wengine wengi tupeni uhondo.

Si lazima kutafsiri vitabu lakini zipo simulizi kuhusu yale mliyoyaona wakati huo, jinsi nchi ilivyoendeshwa, jinsi mabadiliko yalivyokuja na mengine mengi.

Sisemi kwamba hamjafanya kabisa hapana, najua baadhi huandaa vipindi, huandika makala na kufanya mahojiano lakini isiishie hapo, tuandikieni vitabu, vitangazeni ili watanzania wavinunue na waijue nchi yao ilikotoka. Jenerali Ulimwengu nakupongeza pia kwa kuwa umetekeleza hili.

Nasema hivi kwa sababu naamini kuwa, baadhi ya matatizo yanayotukumba sasa Tanzania yanaweza kutatuliwa kwa nguvu ndogo tu ya sisi wanahabari kutumia kalamu zetu kuwapata taarifa watanzania, kuwakumbusha watanzania na kuwaonesha njia ya kupita.

Leo hii inashangaza kumuona mtanzania akitoa kipaumbele kwa mambo ambayo yanaibomoa nchi, yanavuruga moyo wa kuijenga nchi kwa kujitolea, yanajenga chuki, yanaruhusu wabaya kuivuruga nchi. Tulikotoka haikua hivyo, na nchi za wenzetu kama vile China bado wanafanya yale ambayo sie tulikua tunayafanya kabla ya miaka ya 90.

Najua aya hiyo hapo juu itakua imewachefua baadhi ya watu, lakini niseme sababu hizo zinazotumiwa na baadhi yetu kuhalalisha mambo yanayoigharimu nchi utatuzi wake unapaswa kutenganishwa na jukumu la msingi la kujenga Taifa letu.

Kama kuna wezi, mafisadi ama walafi tuwaache washughulikiwe na vyombo husika. Wasiohusika tukazane kujenga nchi, haiwezekani sote tukawa walalamikaji, sote tunatafuta wala rushwa na wezi na mwisho wa siku sote tukawa wanasiasa. Nchi atajenga nani?

Jamani eheee wakongwe wa Habari andikeni vitabu watanzania wasome enzi za mwalimu watanzania waliishi vipi?

Na je wala rushwa hawakuwepo?

Mafisadi hawakuwepo?

Viongozi legelege hawakuwepo?

Siasa hazikuwepo?

Waaminisheni watanzania kuwa kila mtu anaweza kuwa mpigania nchi yake na akawa shujaa, kama ambavyo Mjengwa amemuandika Mzee Madiba na simulizi nyingi nyingi alizowahi kuandika.


Mwisho nawapenda sana na niliyoandika sio msahafu.