Kwanza nawapongeza
wapiganaji wote tunaoendelea kufanya kazi ya uandishi wa habari ambayo kimsingi
ni kazi ya kiutumishi kwa umma.
Naomba tuendelee
kutumikia umma wa watanzania na tuendelee kuandika habari zenye maslai kwa
umma. Kwangu mimi utumishi wetu utakua na maana na manufaa kwa watanzania kama
tutaandika, kutangaza, kuonesha na kuchapisha habari, taarifa na matangazo
yenye kuitetea Tanzania na watu wake.
Kwenye kazi ya
kuitetea Tanzania na watu wake tusisahau kwamba zipo taarifa nyingine ama
habari nyingine licha ya ukweli wake na ubora wake zina madhara kwa Tanzania na
watu wake, kwa aidha kuichafua nchi usoni kwa mataifa mengine ama zinawaathiri
watanzania.
Naamini tunayajua haya
na wengi tunayatekeleza, hebu tuendelee kufanya hivyo na wale wasiofanya oneni
umuhimu wa kufanya hivyo ili Tanzania iwe mahali salama pa kuishi na watanzania
wafurahie maisha yao licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi ikiwemo umasikini.
Tukiwa tunakumbushana
hili hebu pia tukumbushane umuhimu wa kuzingatia weledi, maadili, haiba na
staha ya mwandishi wa habari. Tusione haya kujifunza, tusione makosa kukosoana
na isiwe hatari kukubali pale unaposhindwa.
Nasema hivyo kwa
sababu wapo baadhi yetu ambao kimsingi hata wao wanajua kwamba kazi hii
haiendani nao lakini wanalazimisha, matharani kuwa watangazaji bila kujali
ubora wa sauti, rafudhi na uwezo wao kiutangaza, wapo wanaofanya uchambuzi
magazetini kwenye redio na Televisheni bila kujali kama uchambuzi wao hauna
utafiti wa kutosha wala mpangilio, wapo wanaokwenda kukusanya habari bila
kujali muonekana wao mbele ya jamii na tabia zao kama zinafanana na kioo cha
jamii na wapo wanaochapisha magazeti na vijarida bila kujali yale
wanayochapisha kama yana tija ama la.
Nasema bahati nzuri,
haya ninayosema sie wenyewe wahusika tunayajua, nashauri tupime wenyewe na
kuchukua hatua kabla ya kuhukumiwa na jamii ama kusubiri tupigiwe kelele.
Na sasa tunakwenda
kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadaye Uchaguzi Mkuu na tayari
hekaheka zimeanza leo, nashauri tutumie kalamu zetu kukataza hekaheka hizi kwa
sababu zina madhara kwa taifa, muda wake bado japo wapo watakaonikosoa. Tunaliacha
taifa liwe linatumia muda mrefu kujadili uchaguzi badala ya maendeleo,
tunaliacha taifa ligubikwe na ajenda ya siasa badala ya kupambana na umasikini
unaowatafuna watanzania wengi, tunaacha watu wachache wanaotetea maslai yao
kuliyumbisha taifa na mwishowe tunawaacha watanzania washindwe kutengeneza
ajenda za nchi yao. Ndio, ni sisi waandishi wa habari tunaopaswa kuwajibika kwa
hili anayekataa atupishe.
Napiga la Mgambo
nikiomba waandishi wenzangu tuwe chanzo cha matumaini kwa watanzania, tusiache
nchi ikitupiwa mawe ndani na nje, tusiache matatizo ya watanzania yakawa donda
ndugu, na tuwaongoze watanzania kukataa jambo lolote linaloigharimu nchi na
watu wake kwa njia ya amani.
Mwisho nawapenda sana
na Aluta Continua………..