Friday, March 29, 2013

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lapitisha kuanzishwa kwa kikosi cha uingiliaji nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jana lilikubali kutumwa kwa kikosi cha uingiliaji ili kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya makundi ya waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 

Nchi 15 wajumbe wa baraza hilo lilipitisha azimio la kuanzishwa kwa kikosi hicho chini ya utaratibu wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO. 

Kwa mujibu wa azimio hilo muda wa kikosi hicho ni mwaka mmoja, na kazi yake itakuwa ni kupambana na makundi yenye silaha na kupunguza tishio la makundi hayo kwa serikali ya nchi hiyo na usalama wa raia. 

Kikosi hicho kitakachoongozwa moja kwa moja na MONUSCO kitakuwa na batalioni tatu, na makao makuu yake yatakuwa mjini Goma. 

Tarehe 5 Machi katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw Ban Ki-moon alitaka kiundwe kikosi cha uingiliaji ili kukabiliana na tishio la usalama na amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.