By Baraka Mpenja
Ni vita ya kufa
na kupona kati ya watengeneza sukari nchini Tanzania klabu ya Mtibwa
Sugar dhidi ya Kagera Sugar watakaokuwa na kazi ngumu ya kuwania pointi
tatu muhimu katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Pambano hilo la watengeneza sukari
sukari limevuta hisia za mashabiki lukuki wa soka kwa mikoa ya kanda ya
ziwa Victoria huku likitarajiwa sehemu ya kufurahia katika mapumziko
ya pasaka.
Akizungumza kutoka mkoani Kagera,
kocha mkuu wa Mtibwa sugar na nahodha wa zamani wa timu hiyo pamoja na
timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), mzalendo Merck Mexeme amesema
maandalizi ya mchezo huyo yamefanyika kwao Manungu na leo hii wanapasha
moto misuli baada ya safari ndefu ya siku mbili kuelekea mkoani humo.
Mexme alisema soka siku zote ni
maandalizi, wao wamejipanga vizuri na bahati nzuri hakuna mchezaji
ambaye yuko hatarini kuukosa mchezo huo unaotabiriwa kuwa mgumu sana.
“Kagera ni timu nzuri na wana
kocha mzuri, mzee Abdallah King Kibadeni ambaye alinifundisha hata mimi,
ana mbinu nyingi sana lakini kwa kuwa aliwahi kuwa mwalimu wangu,
nitatumia mbinu zake kumfunga akiwa nyumbani kwake hapo kesho”. Alisema
kocha Mexeme .
Mexeme ambaye ni kocha
aliyejijengea heshima kubwa akiwa mchezaji na sasa kocha wa Mtibwa sugar
aliongeza kuwa kesho atapanga kikosi chake cha matumaini na anawapanga
vijana wake kupambana na Kagera Sugar ambao watakuwa mbele ya umati
mkubwa wa mashabiki ambao ndio siri ya matokeo unapocheza uwanja wa
nyumbani.
Naye mshambuliaji mahiri wa
tanzania miaka ya nyuma huku akivuma na kupewa jina la king Mputa akiwa
na klabu ya Simba akicheza kama winga mahiri miaka ya sabini na sasa ni
kocha wa watengeneza miwa pacha wa mtibwa, Kagera Sugar “
wanangulukumbi” Abdallah Kibaden akiongea kwa kujiamini baada ya kutoa
dozi kwa simba SC amesema kuwa mchezo wao wa kesho wanataraji kuwapa
zawadi ya pasaka mashabiki wao.
“Mara baada ya kuifunga simba
goli 1-0, vijana wangu wana kila sababu ya kuongeza wigo wa tofauti ya
pointi kati yetu na Mtibwa ,Wanahitaji sana ushindi katika mchezo wa
kesho, malengo yetu ni kupata nafasi mojawapo ya kuwakilisha nchi
medani ya kimataifa”. Alisema king Mputa.
Nao mabingwa watetezi wa taji
wekundu wa Msimbazi Simba “Taifa Kubwa” baada ya kipigo cha 1-0 sasa
watakuwa na kazi pevu katika nyasi nzuri za uwanja wa CCM Kirumba
kudadavuana na watoto wa mitaa ya Kishamapanda Toto Africa.
Simba watashuka Kirumba wakitaka
kuonesha uwezo wao na manjonjo ya vijana wake mbele ya mapacha hao wa
vinara wa ligi kuu ya kandanda Tanzania bara, klabu ya Yanga ya Dar es
Salaam.
Tayari timu tatu za Mbeya city ya
jijini Mbeya, Ashant United ya Dar es Salaam na Rhino Rangers ya Tabora
zimeshakata tiketi ya kucheza mitanange ya ligi kuu msimu ujao, huku
timu tatu za ligi zikisubiri kupitiwa na fagio la chuma.
Timu za African Lyon, Polisi
Morogoro, JKT Ruvu, Tanzania Prisons, Mgambo shooting na JKT Oljoro
zinaonekana kuchuana vikali kukwepa mkasi wa kurejea ligi daraja la
kwanza Tanzania bara (FDL).