Monday, August 12, 2013

Majimaji Sports Club sasa kuwa Kampuni

Wadau walioshiriki Mkutano ulipokea taarifa ya Majimaji Sports Clu kuwa Kampuni

Na; Msigwablog 
Hatimaye wadau wa timu ya Majimaji ya Songea almaarufu Wanalizombe wameamua kuwa timu hiyo iwe kampuni na itakayokua ikiuza hisa zake katika soko la Hisa la Dar es salaam (DSE)

Haijafahamika hisa moja itauzwa shilingi ngapi na kutakua na hisa ngapi lakini kulingana na maelezo ya wadau walioandaa mkutano huu yaani Kampuni ya Tanzania Mwandi hatua hiyo inalenga kukabiliana na changamoto kuu ya timu hiyo ambayo ni ukata.

Silas Mwakibinga ambaye ni Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania TFF anasema sasa wawekezaji mbalimbali wanaweza kununua hisa, kama  inavyofanyika kwa timu za ligi kuu nchini Ulaya hali ambayo itaiwezesha timu hiyo kujiimarisha kiuchumi ikiwemo kuwa na uwanja wake, kusajili wachezaji wazuri na kuwaandaa vizuri kwa mashindano na pia itakua na uwezo wa kufanya biashara.

Mwakibinga anasema tayari baadhi ya wawekezaji wameshaonesha nia ya kununua hisa nyingi na kuwekeza katika timu ya Majimaji wakiamini kuwa mfumo huo unalipa na Majimaji itakua katika nafasi nzuri ya kuwa timu bora zaidi katika timu za soka za Tanzania Bara.

Akiwasilisha Mada kwa niaba ya Mwanasheria Dr Damas Ndumbaro, mwanasheria Abel Ngilangwa anasema kwa kuwa Kampuni sasa Majimaji Sports Club itakua imeachana na mfumo wa kuwa mali ya wanachama na sasa itakua ni mali ya wanahisa na kwamba mwenye hisa nyingi zaidi ndiye atakayekua na sauti zaidi kwenye Kampuni.

Mdau mwingine wa Soka ambaye pia ni mwanasheria Sebastian Walyuba amewashauri wapenzi wa timu ya Majimaji na wanaruvuma kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kununua hisa kwa kuwa hiyo ndio njia pekee itakayowawezesha kushiriki katika timu hiyo vingine watatupwa nje.

Mapema akifungua Mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alisema mfumo huo ni mzuri na akatoa changamoto kwa uongozi wa Kampuni ya Majimaji kuhakikisha timu inashinda katika mechi zake na kwamba kwa kufanya hivyo ndio njia pekee itakayowavutia wawekezaji wengi kuweka pesa zao katika Kampuni hiyo
.........................