Wednesday, July 10, 2013

CHEMBA YA MADINI NA NISHATI INAUNGA MKONO MRADI WA MATOKEO MAKUBWA SASA

Prof.-Sospeter-Muhongo
Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo
Dar es Salaam
Chemba ya Madini na Nishati Tanzania, inaipongeza serikali kwa kuanzisha Mradi wa Matokeo Makubwa Sasa. Baada ya kushuhudia uzinduzi wa miradi ya kitaifa katika sekta ya nishati uliofanywa na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, uzinduzi uliofanyika Mlimani City tarehe 3 Julai, 2013, Katibu Mtendaji wa TCME alisema, “wajumbe wetu katika tasnia ya madini wanafuatilia kwa makini maendeleo katika sekta ya nishati kwa sababu ya mabadiliko yatakayosababisha kwenye maendeleo ya sekta ya madini. Tunaipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa jitihada na ahadi hizi za utekelezaji.”
Makampuni ya uchimbaji madini Tanzania ni mojawapo ya watumiaji wakuu wa nishati nchini, lakini mara nyingi yanahitajika kutengeneza nishati yake kwa kutumia mashine makubwa na ghali ya kutumia mafuta. Upanuzi wa gridi ya taifa kuelekea Kaskazini Magharibi mwa Tanzania kutafanya uchimbaji madini kuwa uwekezaji wa kuvutia zaidi. Masuala mengine yote yakiwa sawia, migodi iendeshwayo kwa nishati ya uhakika ya gridi ya taifa inapunguza gharama kwa wazalishaji na kuwawezesha kujenga migodi zaidi na kupanua miundombinu ambayo tayari wanayo, na hii inapelekea utengenezaji wa ajira na inaongeza malipo ya kodi kwa serikali.
“Matokeo Makubwa Sasa ni hatua ya bashasha sana” Bwana Jengo alisema, “ Tuna uhakika kuwa kwa pamoja, wenzetu serikalini na wale wa sekta binafsi tutafanikisha manufaa ya moja kwa moja na yanayoshikika kwa Tanzania na jamii yetu ya kibiashara. Inawezekana endapo kila mmoja wetu atatekeleza katika nafasi yake.
“Mradi wa Matokeo Makubwa Sasa hauishii kwenye umeme. Makampuni ya uchimbaji madini na nishati yanafurahishwa na maboresho ya miundombinu. Bandari bora zaidi, barabara zilizoboreshwa na reli zilizowekwa katika hali nzuri zitasaidia kuongeza ari ya uwekezaji katika nchi yetu. Imani kwa miradi mingi ya ndani ambayo wanachama wetu wanazifanyia kazi itaongezeka tu kwa uwepo wa usafiri wa kisasa na uboreshaji wa uwezekano wa maendeleo.”
Huku uchimbaji madini ukiwakilisha zaidi ya 3% ya kipato cha ndani cha Tanzania, na dhahabu pekee ikiwakilisha 50% ya mauzo ya Tanzania nchi za nje, sekta hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa. Kuna matarajio makubwa kuwa mradi wa Matokeo Makubwa Sasa utasaidia tasnia ya uchimbaji madini ambayo, nayo, itasaidia uchumi wa Tanzania.