Na Miza Kona-Maelezo Zanzibar
Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imeendelea na msimamo wake wa
kuwahahakikishia Wazanzibari kuwa itasimamia na kuyatekeleza matakwa yao
watayokubaliana katika Mabaraza ya Katiba ili kupata Katiba Mpya yenye
kukidhi mahitaji yao.
Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Abubakar Khamis Bakary ameyasema
hayo wakati akisoma hotuba ya Makadirio ya Mapato na matumizi ya Wizara
yake mwaka wa fedha 2013/2014 Katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi
Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Amesema jambo la msingi kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni kufanya
maamuzi ya kujua wanataka Muungano wa aina gani na Katiba ipi ili
Wananchi watakapoenda kutoa Maoni yao katika Mabaraza ya Katiba wawe na
hoja za msingi.
“Kwanza ni sisi wenyewe kujua tunataka Muungano upi na Katiba ipi kasha tuwaelimishe wananchi wetu”Alisema Waziri Bakary.
Amesema Wanachi wasiwe na wasiwasi na kwamba kupitia kwa Wawakilishi wao
waijadili Rasimu ya Katiba na kuona kama inakidhi haja ya kuleta
Maendeleo, Maisha mazuri na haki za Wazanzibar kwa kizazi kilichopo na
kijacho.
“Tuhakikishe kuwa Katiba ijayo inafufua matarajio ya Wazanzibari kwa Zanzibar yetu ya leo na siku za usoni”alisema Waziri Bakary
Aidha Waziri Bakary ameitaka jamii kufahamu kuwa Katiba inayotakiwa
itabadilisha sana Taifa kisiasa, kiuchumi na kijamii na kwamba Wananchi
wanatakiwa kuwa imara na mazingatio ya mabadiliko hayo.
Alieleza kuwa mabadiliko yatakayotokana na Katiba Mpya yanaweza kuwa ya
karibuni na mengine kuchukua muda mrefu hivyo wananchi wajitayarishe
kukabiliana nayo
Katika hatua nyingine Waziri Bakary amesema Wizara yake kupitia Idara ya
Mahkama imepanga kupunguza mrundikano wa kesi na kuongeza ufanisi
katika utoaji wa haki.
Aidha Majengo ya Mahkama ya Unguja na Pemba yanatarajiwa kufanyiwa matengenezo ili kuyapa hadhi ya kisasa.
Katika kutekeleza majukumu yake Waziri huyo ameliomba Baraza la
Wawakilishi limuidhinishe jumla ya sh. 8,188,000,000.00 kwa matumizi ya
kazi za kawaida.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR