------------------------------------------
Na Nathan Mtega,Tunduru
Serikali wilayani Tunduru
mkoani Ruvuma imewataka wananchi na
viongozi wa serikali na vyama vya siasa wilayani humo kutambua kuwa jukumu la uhifadhi
na utunzaji wa mazingira ni la kila
mmoja kwa sababu madhara ya uharibifu wa mazingira yanaathiri kila kundi.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa
wilaya ya Tunduru Chande Nalicho wakati akifungua mdahalo
wa wazi wa mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi juu ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya
hali ya hewa ambapo amesema tabia , shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya hali
ya hewa ni vitu vinavyochangia uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa.
Amesema kuwa mdahalo huo unaoendeshwa na asasi ya kiraia ya
mazingira Tunduru kwa ufadhili wa asasi ya The foundation for
civil society una lengo kubwa la kuikoa wilaya Tunduru
dhidi ya uharibifu wa mazingira unaozidi kuongezeka siku hadi siku.
Amesema kuwa shughuli mbali mbali
za kibinadamu pamoja na kilimo kisichozingatia ushauri wa kitaalamu ambacho huhusisha
kilimo cha kuhama hama kinachofanywa na baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo huku
wataalamu wa sekta ya kilimo wakishuhudia bila kuchukua hatua za kutoa elimu na
ushauri wa matumizi bora ya ardhi ni sababu zinazosababisha kuendelea kuwepo
kwa uharibifu wa mazingira siku hadi siku.
Akiongoza mdahalo huo mwezeshaji
Thomas Lima amesema kuwa sera ya taifa ya mazingira inasisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira
lakini elimu zaidi kwa wananchi na sheria za utunzaji na uhifadhi wa mazingira
vinapaswa kuzingatiwa kwa sababu sekta ya uhifadhi wa mazingira imekuwa
ikifadhiliwa kwa gharama kubwa na wafadhili wa ndani na nje ya nchi.
Amesema kuwa suala la uhifadhi wa mazingira
linapaswa kupewa kipaumbele kuanzia ngazi ya familia ili kuwajengea watoto
utamaduni wa kuyapenda na kuyatunza mazingira yanayowazunguka kwa sababu moja
ya sababu zianazochangia kuendelea kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira ni
pamoja na ukosefu wa elimu ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa wananchi
walio wengi na hasa waliopo maeneo ya vijijini ambako hutumia kuni kama nishati
kwa kukata miti bila kupanda.
Akizungumza mratibu wa asasi hiyo
ya kiraia ya mazingira Tunduru John Nginga amesema kuwa mdahalo huo
uliofunguliwa na mkuu wa wilaya
hiyo ya Tunduru utafanyika katika majimbo
mawili yaliyopo wilayani Tunduru ambayo ni Tunduru kaskazini na Tunduru kusini
kwa lengo la kuikoa wilaya hiyo na uharibifu wa mazingira unaozidi kukua kwa
kasi kubwa siku hadi siku.
Habari kwa hisani ya demashonews