Wednesday, July 10, 2013

WADHAMINI TAIFA STARS WALETA MATUMAINI MAPYA

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe akimpa zawadi Nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja baada ya chakula cha jioni jana 
Na Michael Mukunza, 
  WADHAMINI wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kilimanjaro Premium Lager, wamewataka Watanzania kutokata tamaa licha ya Taifa Stars kutofuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia Brazil mwakani kwani timu imeonesha uwezo wa hali ya juu mpaka sasa. Ombi hilo lilitolewa na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe wakati alipowaandalia Taifa Stars chakula cha jioni katika hoteli ya Tansoma ikiwa ni utaratibu wa wadhamini hao kama njia ya kuwakaribisha wachezaji kambini.
Alisema bado kuna mashindano mengne kama CHAN na AFCON ambayo wana imani Taifa Stars itafuzu na kwuweka historia. Aliwaasa wachezaji kuhakikisha wanashinda mechi dhidi ya Uganda haa nyumbani na pia watakapoenda Uganda baadaye mwezi huu katika mechi ya kuwania kufuzu mashindano ya CHAN mwakani nchini Afrika Kusini. “Tumeshindwa kufuzu kwenda Brazil basi twende Afrika Kusini mwakani,” alisema Bw. Kavishe. Alisema wao kama wadhamini wamefarajika kuona jinsi Timu ya Taifa imepiga hatua tangu waanze kuidhamini mwaka jana. “Vilabu vya  Simba na Yanga zilikuwa na nguvu sana na moja ya dhamira zetu kama wadhamini ilikuwa ni kuinua kiwango cha Taifa Stars na kufanya watanzania warudishe imani kwa timu yao na sote ni mashuhuda kwani katika mechi ya kwanza kabisa mwaka jana uwanja ulikuwa na watu 10,000 tu lakini katika mechi dhidi ya Ivory Coast hivi majuzi uwanja ulijaa kabisa,” alisema. Meneja huyo pia alitumia nafasi hiyo kutoa zawadi maalumu kwa wachezaji hao ambazo ni pamoja na DVD zilizorekodiwa maelezo (profiles) za kila mchezaji, kazi ambayo ilifanywa kitaalamu kwa udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager. Wachezaji wataweza kutumia kazi hizi kwenye mitandao ili waweze kujulikana vizuri ndani na nje ya nchi.
Mwinyi Kazimoto anapokea mzigo

Shomari Kapombe..

John Bocco

Nadir Haroub 'Cannavaro'

“Tulisema tunaijenga timu na timu inajengwa na wachezaji na ndio maana tumeamua kufanya kazi kama hizi ambazo zitapandisha hadhi ya wachezaji,” alisema huku akitoa wito kwa vilabu kutosita kuaruhusu wachezaji wakati wanaitwa kurekodi kazi kama hizo. Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa, Kim Poulsen aliwashukuru wadhamini na kusema, “Kwa kweli mumekuwa zaidi ya wachamini maana ushirikiano mliioonesha ni wa hali ya juu.” Alisema wachezaji wana ari kubwa sana kwani matunzo wanayopata sasa hivi ni ya hali ya juu na wote wanalenga kupata mafanikio. Taifa Stars iko kambini kuanzia Julai 4 mwaka huu ikijiandaa na mechi dhidi ya Uganda Jumamosi hii na mechi ya marudiano itapigwa wiki mbili zijazo Mjini Kampala ili kuwania kufuzu katika mashindano ya CHAN.