Monday, July 8, 2013

Muhimu!!!!!! Wingu kwa waandishi wa Habari Tanzania


Ujumbe kwa Wadau.

Moja ya mambo yanayoniumiza kichwa juu ya tasnia hii ya uandishi wa Habari ni jinsi Agenda hii ya “MASLAI KWA WAANDISHI WA HABARI YANAVYO FYONZA TAALUMA HII” Nimeandika kwa herufi kubwa kwa lengo la kutia Msisitizo tu.

Swali gumu; Hivi ni nani anayewajibika kumtetea mwandishi wa habari?

Kwangu swali hili naliona gumu kwa sababu mbele ya macho yangu swali hili limefunikwa na wingu zito kiasi kwamba wanaopaswa kulipatia majibu pengine limewafunika.

Nakumbuka miaka kumi na tatu iliyopita, mmoja wa wanasiasa wakongwe hapa Nchini Dr Laurence Mtazama Gama, (Mungu ailaze roho yake pema peponi) aliwahi kuniita nyumbani kwake pale jirani na Ikulu ndogo ya Mkoa wa Ruvuma na akaniambia hivi, “Mwanangu unaanza kazi hii ya uandishi wa habari, kazi hii inataka ujasiri mkubwa, sio kazi ya kusifia sifia tu mara waziri, mara mkuu wa Mkoa, mara Mkurugenzi hapana!!! Ni kazi ya kuwapigania wananchi kwa kufichua mambo ambayo aidha yanafanywa makusudi ama bila makusudi ili yatafutiwe ufumbuzi”

Akaongeza kuwa “kwa wakati huu lipo tatizo la pesa za umma kutumiwa vibaya sana na tabia hii inazidi kupamba moto, sasa mimi nataka nikupe njia rahisi ya kufanyia kazi tatizo hili. Nazo ni kwanza katika Halmashauri za wilaya au mji ukiona Mwenyekiti wa Halmashauri au Meya wanapatana sana na Mkurugenzi basi ujue wanashirikiana kula pesa za umma, Ukiona Mkuu wa Mkoa wanaelewana sana na Katibu Tawala wake basi ujue pesa za Mkoa zinaliwa, hali kadharika ukiona taasisi mbili zinazopaswa kusimamiana, viongozi wake wanauswahiba wa kupitiliza basi ujue wanajinufaisha”

Dr Gama aliyasema haya akinukuu tabia zilizoshika mizizi kwa wakati huo za viongozi na watendaji wakuu katika vyombo vya umma kutanguliza maslai binafsi.

Kwa kuzingatioa kauli hii ya Dr Gama, naviangalia vyombo vinavyohusika na waandishi wa habari yaani Baraza la Habari (MCT), Jukwaa la Wahariri (TEF), Wamiliki wa vyombo vya Habari (MOAT), Umoja wa vyama vya waandishi wa Habari (UTPC) na vinginevyo.

Najiuliza

1.     Ni kwa kiasi gani vyombo hivi vinasimamiana?

2.    Ni kwa kiasi gani vyombo hivi vinapigana kuondoa maslai duni ya waandishi wa habari?

3.    Mbona kundi la waandishi wa habari choka mbaya haliishi?

4.    Mbona sioni matumaini kwa tasnia hii ikilinganishwa na wenzetu km walimu, madakrtari nk?

5.    Mbona bado mwandishi wa habari analipwa shilingi 3,500/- kwa story?

6.    Mbona waandishi wengi hawana ajira, hawana mikataba na wanaendelea kutumika?

7.    Na mengine mengi.

Mimi nilidhani vyombo hivi tungekua tunasikia kila kukicha vikipambana tena kwa uwazi kupigania hali za waandishi wa habari, tusikie wamiliki wa vyombo vya habari wanabanwa kulipa vizuri waandishi wao, tusikie wamiliki wanashinikizwa kuwaendeleza kitaaluma waandishi wao, tusikie mapesa ya wafadhili yanatolewa maelezo ya kina juu ya namna yanavyotumika kwa maslai ya mwandishi wa habari, tusikie mapambano makali ya kuhakikisha vyombo vya habari vinazingatia ubora wa habari. Na mengine mengi.

Nimekaanalo moyoni kwa muda mrefu na sasa nimeamua nifungue mjadala kwa mara nyingine. Mimi naamini hakuna Weledi wenye mafanikio ndani changamoto lukuki zinazowakabili waandishi wa habari.

Angalizo tuepuke Jazba, tujadili kwa manufaa na tuchukue hatua stahili zinazofanana na maadili yetu hasa ikizingatiwa sisi ni kioo cha Jamii na Mhimili wa nne wa dola usiorasmi.

Natoa Hoja.