Wednesday, May 1, 2013

MAGUNIA MENGINE SITA YA BANGI YAKAMATWA ARUSHA

GEDSC DIGITAL CAMERA
Hizo ndio dawa zenyeweGEDSC DIGITAL CAMERA
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Mapambano dhidi ya uzuiaji wa madawa ya kulevya mkoani Arusha yanazidi “kupamba moto” baada ya jeshi la Polisi Mkoani hapa kukamata gari lililokuwa na magunia sita ya bangi. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa mwezi wa April muda wa saa 6:00 Mchana wilayani Longido.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas alisema tukio hilo lilifanikiwa baada ya askari wa jeshi hilo kupata taarifa toka kwa raia wema juu ya kuwepo kwa tukio la kusafirisha madawa hayo toka Longido Mjini kuelekea Namanga.

Alisema askari walipopata taarifa hiyo walianza kulifualia gari hilo aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T. 526 BWX na mara baada ya dereva wa gari hilo kugundua anafuatiliwa aliamua kulitelekeza na kisha kukimbia.
“Mara baada ya askari kulifikia gari hilo walilipekua na kukuta gunia sita za madawa ya kulevya aina ya bangi zikiwa nyuma ya siti na mpaka hivi sasa mmiliki wa gari hilo bado hajajulikana na tunafanya juhudi za kumtafuta”. Alisema Kamanda Sabas.

Aidha kwa upande mwingine Kamanda Sabas aliendelea kuwashukuru baadhi ya wananchi wa Mkoa huu kutokana na ushirikiano mzuri juu ya utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa jeshi hilo hali ambayo inasaidia kuzuia vitendo vya uhalifu na kukamatwa kwa wahalifu wa matukio mbalimbali.
 Aliendelea kuwasihi wakazi wa mkoa huu na mikoa mingine hapa nchini kuendelea kushirikiana na jeshi hilo katika kupeana taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuweza kuzidi kuimarisha hali ya amani na utulivu.