Friday, May 3, 2013

Neno La Leo; Tunapoitafakari Siku Ya Uhuru Wa Vyombo Vya Habari Duniani...

Ndugu zangu,

” Maisha yetu huanza kuisha siku tunapoanza kunyamaza kwenye mambo yenye maana”- Martin Luther King Jr.


Leo Mei 3 ni Siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari  Duniani. Hapa Afrika Mashariki, siku hii inaazimishwa kule Arusha kwa Kongamano lililoandaliwa na Mfuko wa  Ruzuku kwa Vyombo Vya Habari ( TMF).


Macho na masikio yetu yanaelekezwa Arusha. Maana, kule Arusha kunatarajiwa kuzinduliwa kwa Itifaki ya Vyombo Vya habari.  


Ndio, kuna  Azimio la Arusha linakuja, lakini hili linawahusu Wanahabari. Na kauli mbiu ya Siku hii ya Vyombo Vya Habari ni ” Mazingira  Mazuri na Salama ya Kufanyia Kazi Kwa Wanahabari wa Afrika Mashariki”. 


Ni ukweli, kuwa mwanahabari hawezi kuwa huru kwenye mazingira mabaya na yasiyo salama ya kufanyia kazi. Lakini, kuna maswali ya kujiuliza na kutafakari kwa kina. Ni  natumaini yetu walio kule Arusha wataifanya kazi hii ya kufikiri. Wafanye hivyo  ili Azimio watakalotoka nalo Arusha liwe lenye maana kwa wanahabari na umma unaowatumikia.


Na mwanahabari anapokuwa hana uhuru wa kiuchumi kimsingi anawekwa kwenye mazingira mabaya na yasiyo salama ya kufanyia kazi. 


Hakika, Media ni mhimili muhimu sana katika nchi yeyote inayotaka kupiga hatua za kweli za maendeleo. Hata hivyo, katika nchi zetu hizi, media imefanywa kuwa adui wa watawala na hivyo basi, wakati mwingine kumekuwa na mahusiano ya uhasama, kuviziana  na kuwindana.


Na kwa umma, media nayo ina sehemu yake ya lawama pale inaposhiriki kubomoa badala ya kujenga misingi ya Utaifa na Ujenzi wa Taifa Huru lenye nguvu za kiuchumi. Ni pale, inaponyamaza kwenye mambo ya maana na kushabikia yasiyo na maana, yenye kupotosha na kusababisha chuki na migongano katika jamii.  Mathalan, udini, ukabila na mambo ya  abrakadabra kama vile ndoto za Babu wa Loliondo na Kikombe chake.


Na hakika hili huchagizwa pale Media inapoingiliwa na wanasiasa, wafanyabiashara na hata baadhi ya viongozi wa dini. Ni matokeo ya Media kukosa uhuru wa kiuchumi. Ni wakati sasa wa vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla wake, kudai haki za kuwa na trade unions zake zenye meno. Kudai pia haki ya kupewa ruzuku na Serikali inayotokana na kodi za wananchi ili vyombo hivyo viweze kujijengea uwezo zaidi katika kuitumikia jamii. Media ya nchi haiwezi kuishi kwa kutegemea ruzuku inayotokana na walipa kodi wa Ulaya na Marekani. Ni fedheha pia.


Ndugu zangu,

Mengine tunayoyashuhudia siku hizi  ni  kwa baadhi ya vyombo vya habari  kushabikia mambo yasiyo na maana na kunyamazia yale ya msingi. Hii ni hatari kwa mustakabali wa nchi zetu hizi. 


Na tusije kusahau kuwa umma bado una imani kubwa kwa media. Hivyo, kuna umuhimu wa kuzingatia maadili.  Inahusu virtue, kwa maana ya maadili na kutenda yalo ya haki. Kutenda yalo mema. 


Mtu mwenye maadili mema utamwamini, ndivyo pia wasemavyo Waingereza; a virtuous person  is someone you can trust. 

Mzazi anapaswa kuwa a virtuous person, kiongozi wa kisiasa anapaswa kuwa a
virtuous person, kiongozi wa kidini anapaswa kuwa a virtuous person,  Mwandishi wa habari anapaswa kuwa a virtuous person. Vivyo hivyo kwa mwalimu.
Ndugu zangu,
Wanahabari wa Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu wao uliopita wameonyesha kuwa inawezekana, kwa Media kutanguliza maadili, kuachana na yasiyo na maana na kujielekeza kwenye yaliyo ya msingi na yenye kulinda Umoja na Utaifa wao.

Na katika haya ya kushabikia yasiyo na maana, kuna wakati Julius Nyerere alitua Jomo Kenyatta Airport. Hapo aliongea na wanahabari. Ni miaka ile ya mwanzoni mwa Uongozi wa Rais Mwinyi baada ya Nyerere kung’atuka. Enzi za Mwinyi kuna mambo yaliyoonekana yana nafuu zaidi. Kukawa na minong’ono, kuwa  eti Julius Nyerere anamwonea wivu Mwinyi na ana mipango ya kumwondoa madarakani.


Pale Jomo Kenyatta mwanahabari wa Kenya akamwuliza Nyerere: ” Mwalimu tunasikia unapanga njama za kumwondoa Mwinyi madarakani na hata Rais Moi wa hapa Kenya!”


Julius Nyerere alijibu, ” Hivi wewe ukiambiwa mimi natembea na mama yako, utakimbilia kwenda kuandika habari hiyo?!”


Naam, tunajifunza nini kwenye jibu hilo la Julius Nyerere?


Kwamba kwenye falsafa tunaambiwa, kuwa unapoletewa jambo kuna matatu ya kuyaangalia na kuyazingatia: Udadisi wa uhalisia wa jambo lenyewe (Reasoning), Mantiki ( Logic) na Ulinganishi wa nadharia ( Metafisiki)


Hivyo basi, unapokutana na mtu akakuambia kuwa alipokuwa akitembea  jana usiku, njiani alimwona mbwa akimtafuna mbwa mwenzake, basi, unachopaswa kufanya ni kutulia na kutafakari. 


Yumkini usiku huo mtu huyo alikuwa akitoka kwenye kilabu cha pombe, na kwenye ulevi wake, paka aliyemwona akigombana na paka mwenzake,  kwake ilikuwa ni mbwa anayemtafuna mbwa mwenzake!

Happy Media Day!Maggid Mjengwa,Iringa.0754 678 252