Mkuu wa Mkoa Ruvuma Saidi Thabiti Mwambungu.
Na Nathan Mtega,Mbinga.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amelazimika
kuufunga kwa muda mgodi wa makaa ya mawe wa kampuni ya TANCOAL baada
ya wananchi wa kijiji cha Mtunduwalo kata ya Ruanda Wilaya ya Mbinga kumtaka
aufunge mgodi huo mpaka watapolipwa madai yao ya muda mrefu ya fidia pamoja na
kuyaweka mazingira yao katika hali inayostahili kwa matumizi ya binadamu.
Mwambungu alichukuwa uamuzi huo kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Mtunduwalo ambao ulihudhuriwa na
mamia ya wanakijiji hicho wakiwemo viongozi wa kamati za ulinzi na usalama za
Wilaya ya Mbinga na Mkoa pamoja na
viongozi wa vyama vya siasa.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga
akimkaribisha Mkuu wa Mkoa Mwambungu ili aweze kuongea na wananchi kuhusu
mgogoro uliopo kati ya wananchi na mwekezaji wa mgodi huo ndipo alipoanza kwa kusema wananchi wa Mtunduwalo
hoyee!wananchi wakajibu hoiiii!mpaka kieleweke kadhalika kwa mkuu wa Mkoa
ambapo aliwataka kuwa watulivu wakati anapotaka kuwaambia nini serikali yao
imefanya katika kulimaliza tatizo hilo.
Pamoja na Mkuu wa Mkoa kujaribu kuwatuliza wanakijiji hao
lakini bado hali iliendelea kuwa mbaya baada ya wananchi hao kumshinikiza mkuu
huyo wa Mkoa waende nae mpaka kwenye eneo la mgodi akaufunge na kama
haitawezekana basi wapo tayari kufa kwa kupigwa risasi kuliko kufa kwa njaa
wakati haki zao zipo zinadhurumiwa na viongozi wa serikali huku baadhi yao
wakiugua magonjwa mbalimbali kutoka kunywa maji yenye chembechembe ya sumu ya
madini ya makaa yam awe yanayochimbwa eneo la kijiji hicho.
Akitoa kero mbele ya Mkuu wa Mkoa Mwambungu mwananchi Erick
Mapunda alisema kuwa wamechoka na ahadi hewa za mwekezaji ambazo kila kukicha
imekuwa ni siasa hivyo ujio wa Mkuu wa Mkoa huyo uwe ni hitimisho la kwenda
kuufunga mgodi huo mpaka hapo watapotimiziwa ahadi walizoahidiwa pamoja na
kuwalipa fidia wanazoidai kampuni ya TANCOAL.
Joseph Messa alieleza kuwa yeye kama mwananchi wa kijiji
hicho ameshakata tama ya maisha kwa sababu hali ya kijiji chao ni mbaya
kutokana na kukosekana kwa miundo mbinu ya barabara,maji,shule pamoja na zahanati
kwani watoto wao wamekumbwa na magonjwa ya kichocho ambayo hawajui
yanasababishwa na nini na kwamba wamekuwa wakinywa maji ya sumu tangu mgodi huo
uanze kufanya kazi licha ya kuwa malalamiko hayo walishapewa viongozi wa
serikali ya kijiji,Wilaya na Mkoa.
Kwa upande wake Benedina Komba alisema kuwa tangu mgodi
huo uanze kufanya kazi wananchi wa kitongoji cha Nkaya walipewa ahadi ya kuhama
maeneo yao kwa muda kwa madai kuwa wataonyeshwa maeneo mengine ambayo wangepewa
fidia ili wakajengee mahali pengine jambo ambalo mpaka sasa halijatekelezeka
huku wakiangaika na watoto kutokana na njaa kwa kuwa eneo walilokuwa wakilima
kuchukuliwa na kampuni hiyo.
Wosteri Mapunda alielekeza shutuma nzito kwa waandishi wa
habari wa Mkoa wa Ruvuma kwa kutoandika habari za mgogoro huo tofauti na
waandishi wa Mkoa wa Arusha ambao wamekuwa wakiandika habari za mgogoro wa
Loliondo ambapo serikali baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari ilihamia
Loliondo ili kumaliza tatizo lililopo na kwa nini Mtutunduwalo ishindikane kwa
muda wa miaka mitatu sasa.
Aidha Johoni Nyimbo alimnyooshea kidole
Mbunge wa jimbo la mbinga mashariki Gaudensi Kayombo na kumkumbusha ahadi
aliyowaahidi wananchi wa kijiji hicho mei 19 mwaka 2011 kwenye mkutano wa
hadhara kuwa endapo wanakijiji hao hawatalipwa fidia wanazodai atajiuzuru nafasi
aliyonayo ya ubunge na kumtaka ajiuzulu nafasi ya ubunge mara moja jambo
ambalo lilimpandisha hasira na baada ya
kauli iyo alilazimika kusimama ili kutoa ufafanuzi wa kauli yake hali ambayo
isababisha kuwapandisha hasira wananchi hao na kuanza kumzomea.
Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Oddo Mwisho naye alikumbwa na
adha ya zomea zomea hiyo baada kusimama na kuanza kujieleza kuhusiana na jitihada za
chama cha CCM na Serikali yake ya Wilaya na Mkoa kuwa kwa muda mrefu wamekuwa
wakifanya mazungumzo kupitia Wizara ya nishati na madini,Shirika la maendeleo
ya Taifa (NDC) pamoja na mwekezaji wa kampuni hiyo ya TANCOAL kwa lengo la
kumaliza mgogoro uliopo kati ya mwekezaji na wananchi.
Kufuatia vurugu zilizojitokeza kwenye mkutano huo mkuu wa
Mkoa Mwambung alilazimika kusitisha mkutano huo kwa muda na kuwataka
wananchi hao warudi eneo la mkutano baada ya nusu saa ili apate nafasi ya
kujadiliana na kamati yake ya ulinzi na usalama na baadae baada ya nusu saa
kupita mkutano ulianza ambapo Mkuu wa mkoa Mwambungu aliwaeleza wanakijiji hao kuwa
amesikia maoni yao na amefikia hatua ya kuufunga mgodi huo kwa muda hadi hapo
madai yao mbali mbali yatakapofanyiwa kazi na kutekelezwa.
Chanzo:www.demashonews.blogspot.com