Mwanamke - anayejiita Sister Phylis
Wanjiru Kamau, raia wa Kitui nchini Kenya akiwa ofisi za kamanda wa
jeshi la Polisi mkoa wa Iringa, baada ya kukamatwa.
Taarifa za kipolisi, za kukamatwa kwa Sister Feki Phylis Wanjiru Kamau.
JESHI la polisi mkoa wa
Iringa limemkamata mwanamke Phylis Wanjiru mwenye umri wa miaka 44 aliyevalia
mavazi ya kitawa wa masister wa kanisa Kathoriki, ambapo baada ya kupekuliwa
amekutwa na baadhi ya vielelezo vilivyobaini kuwa ni tapeli.
Wanjiru ambaye ni raia
wa nchi ya Kenya amekamatwa na jeshi la polisi baada ya masister wenzie kubaini
kama si mmoja wao, kutokana na kushindwa kufanya baadhi ya masuala ambayo
ni msingi wa utawa wao.
Akizungumzia mkasa huo,
kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda amesema mwanamke
huyo kabila lale ni Muwembu wa Kituo nchini Kenya amekamatwa majira ya saa kumi
jioni tarehe 13, katika nyumba hizo za masista zilizopo Ipogolo mjini Iringa.
Aidha Kamuhanda amesema
mwanamke huyo ambaye awali aligoma kutoa maelezo ya kina juu ya ujio wake
nchini Tanzania, katika upekuzi walimkuta na baadhi ya chip (Line) za makampuni
mbalimbali ya simu ya ndani na nje ya nchi.
Kamuhanda amesema Sister
huyo bandia alikutwa pia akiwa na hati za kusafiria (Passport) mbili, moja
ikiwa niya Africa Mashariki yenye namba Ke. 020659 huku hati ya nyingine ikiwa
na jumuiya ya Kenya namba A. 1790366.
Amesema Sister huyo feki
katika hati hizo ilionyesha kuwa alitembelea nchi ya Rwanda, Uganda pamoja na
nchini Tanzania ambapo siku za hivi karibuni alikuwa Mkoani Mara Tarime.
Kamuhanda ameitaka jamii
kuwa makini na wageni mbalimbali, huku akiwaasa kuacha tabia ya kuwaamini watu
kwa muonekano wao, kutokana na mwanamke huyo kutumia njia hiyo ambayo inamfanya
kila mtu kumuamini.