Na Genofeva Matemu – MAELEZO,
Shirikisho
la wakurugenzi wa mashtaka Afrika Mashariki limeazimia kuongeza wigo wa
ushiriki wa kikosi kazi ndani ya shirikisho hilo ili kuwajibika zaidi
na kuweza kupata njia nyingine ya kupanua ushiriki wa waendesha mashtaka
binafsi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, rais wa shirikisho
hilo Martin Ngoga amesema kuongezeka kwa wigo kutasaidia kuleta
ushirikiano wa kutosha na hatimaye kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
“ kwa
kipindi hiki uhalifu umekua na changamoto kubwa sana hivyo kufanya kazi
kwa pamoja kutasaidia kupanua wigo wa kupata mafunzo ya pamoja kwa
wanachama wa shirikisho na kupunguza baadhi ya changamoto hizo”, amesema
Ngoga.
Naye
makamu mwenyekiti wa shirikisho hilo ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Mashtaka kutoka Tanzania Dkt. Eliezer Feleshi amewataka waandishi wa
habari kutokujadili na kushadadia kesi zilizoko mahakamani kwani kesi
ikiwa mahakamani hairuhusiwi kujadiliwa bali kuiachia mahakama kufanya
kazi yake.
Mkutano
wa Shirikisho hilo ulioanza jana umemalizika leo ukiwa umehudhuriwa na
wakurugenzi wa Mashtaka kutoka nchi tano za Afrika mashariki uliokuwa
na lengo la kupitia upya Katiba yao ili kuimarisha umoja wao.