Katibu
mkuu wa Chama Cha Riadha Tanzania, Seleman Nyambui akiongea katika
mkutano na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa wadhamini wa Uhuru
Marathon iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Pembeni ni mkurugenzi wa
Kampuni ya Intellectuals ambao ndiyo waandaaji wa mbio hizo, Innocent
Melleck.
MKurugenzi
wa Kampuni ya Intellectuals ambao ndiyo waandaaji wa mbio hizo,
Innocent Melleck akiongea katika mkutano na waandishi wa habari wakati
wa ufunguzi wa wadhamini wa Uhuru Marathon iliyofanyika leo jijini Dar
es Salaam. Pembeni ni Katibu mkuu wa Chama Cha Riadha Tanzania, Seleman
Nyambui.
Waandishi
wa Habari waliohudhuria mkutano huo wakiwajibika wakati wa ufunguzi wa
wadhamini wa Uhuru Marathon iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
WAKATI
mbio zinazosubiriwa kwa hamu kubwa na watu wengi hapa nchini za Uhuru
Marathon zikitarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu, waratibu wa mbio hizo
wamezitaka kampuni, taasisi au watu binafasi wanaotaka kuzidhamini
wafanye hivyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni
ya Intellectuals walio waandaaji wa mbio hizo, Innocent Melleck alisema
wameamua kufungua milango ya udhamini, ili ziweze kufana zaidi.
Melleck
alisema, wanariadha wengi kutoka ndani na nje ya nchi wameonyesha nia
ya kushiriki mbio hizo zitakazokuwa zikifanyika kila Desemba
zikiambatana na maadhimisho ya sherehe za uhuru wa Tanzania Bara, hivyo
wameona ni bora wafungue milango kwa wadhamini.
“Nadhani
wote mnakumbuka uzinduzi wa mbio hizi za Uhuru, uliofanyika Desemba
mwaka Jana, ukiwa unaashiria kuanza kwa mchakato wa maandalizi ya mbio
zenyewe ambazo zitaanza kufanyika Desemba mwaka huu.
“Mbio
hizi za Uhuru, kama lilivyo jina lake zimeanzishwa ili kuongeza chachu
kwa Watanzania kuwa na moyo wa kulinda amani, umoja na mshikamano wetu.
“Kwa
sasa maandalizi ya awali yanaendelea vizuri, nasi tumeona huu ni muda
muafaka kufungua milango ya udhamini kwa makampuni, mashirika na taasisi
mbalimbali ambazo zitahitaji kushirikiana nasi katika kufanikisha mbio
hizi wajitokeze na kupata taratibu za udhamini,” alisema Melleck.
Alisema
kutakuwa na mbio ndefu za kilomita 42, mbio za kati za kilomita 21 na
zile za kujifurahisha za kilomita 5, hivyo mdhamini anaweza kuchagua
aina ya mbio anazotaka kuzidhamini.
Naye
Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui
alisema, tayari kwa upande wao wamekamilisha vitu vingi ikiwemo
kupendekeza mzunguko wa mbio hizo na kuangalia mambo yote ya kiufundi.
“Tunawaomba wadhamini wajitokeze ili kwa pamoja tuweze kufanikisha mbio hizi zenye malengo mazuri kwa Taifa letu kwa ujumla.
“Mbio
hizi tutazisimamia na kuziendesha katika hadhi ya kimataifa ili
kuhakikisha kuwa zaidi ya kulinda Amani na Umoja wetu, pia tunalitangaza
taifa letu kote ulimwenguni.
“Kwa
kuwa mimi ninaangalia zaidi upande wa ufundi, nichukue nafasi hii pia
kuwasihi wanariadha wa hapa nchini kuanza maandalizi ya mbio hizi,
itakuwa si vyema nafasi za juu zikichukuliwa na wageni, wakati sisi
tunao wanariadha wazuri hapa nyumbani,” alisema.
Uhuru
Marathon ni moja kati ya mbio zinazotarajiwa kuleta mapinduzi mapya
katika riadha, ikiwa pamoja na kukumbusha umuhimu wa kutunza na kulinda
amani tuliyonayo.