"Brass Band" ikiongoza maandamano
kutokea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuelekea
Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kuadhimisha miaka 50 OAU/AU.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), akimkabidhi Mkuu wa Mabalozi
na Balozi wa DRC hapa nchini, Mhe. Juma Khalfan Mpango Mwenge wa Umoja
wa Afrika (OAU/AU) kuashiria kuanza kwa maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja
huo yaliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam
Picha zaidi za maandamano.
Mhe. Membe akishiriki maandamano hayo.
Mhe. Membe, Mabalozi, wananchi na wageni waalikwa wakiwa katika maandamano hayo kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Afrika
Mhe. Membe akisikiliza Wimbo wa Taifa na AU zilizopigwa kuadhimisha miaka 50 ya umoja huo
Picha zaidi wakati wa wimbo wa Taifa
Mhe. Membe, Mabalozi, na Viongozi wengine wakiangalia burudani kutoka
vikundi mbalimbali vya utamaduni vilivyopamba maadhimisho hayo
Burudani ikiendelea.
Kikundi kingine cha burudani kilichopamba sherehe hizo.Picha Zote na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
--
Na Ally Kondo
Umoja wa Afrika (OAU/AU) umepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mjini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 25 Mei, 1963.
Hayo yalisemwa na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K.
Membe (Mb) katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya Umoja huo
iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam tarehe 25 Mei,
2013.
Mhe. Membe alieleza
kuwa, AU imefanikiwa kutimiza lengo la kuzikomboa nchi zote za Bara la
Afrika isipokuwa Saharawi kutoka katika tawala za kikoloni. Alisema
katika kufanikisha hilo, Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa kwani,
Makao Makuu ya Ukombozi ya AU yalikuwa hapa nchini.
Kuhusu Demokrasia na
Utawala Bora katika nchi za Afrika, Mhe. Waziri alisema kuwa AU imeweka
utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa wanachama wake wanaheshimu utawala
wa sheria kwa kuweka sheria kali za kukomesha tabia ya kuingia
madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi. Sheria hizo ni pamoja na;
nchi inayotawaliwa kijeshi kusimamishwa uanachama wa AU, kuwekewa
vikwazo vya kiuchumi pamoja na Kiongozi wa Mapinduzi kutoruhusiwa
kuwania nafasi ya Urais katika uchaguzi wa kidemokrasia.
Kutokana na msimamo
huo, AU imefanikiwa kupunguza matukio ya mapinduzi katika nchi za Afrika
tangu ilipoanzishwa. “Afrika imeshuhudia matukio ya mapinduzi matano
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ukilinganisha na matukio 34
yaliyotokea kabla ya kipindi hicho”. Mhe. Membe alisikika akisema.
Katika kukabiliana na
migogoro inayozuka mara kwa mara katika nchi za Afrika, alisema kuwa, AU
imebadilisha kipengele ambacho kilikuwa kinakataza nchi za Afrika
kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. Hivyo, kutokana na
mabadiliko hayo nchi za Afrika sasa zinaweza kuingia katika nchi
nyingine kulinda amani.
Kwa upande wa
maendeleo ya kiuchumi, Mhe. Waziri alisema kuwa hatua kubwa imefikiwa,
hususan kupitia Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda, kama vile SADC, EAC na
ECOWAS. Hata hivyo alibainisha kuwa, ukosefu wa miundombinu imara kama
barabra na reli, kuunganisha Bara zima la Afrika ni kikwazo katika
kufikia malengo ya kiuchumi kwa nchi nyingi za Afrika.
Sherehe za kuadhimisha
miaka 50 ya Umoja wa Afrika (OAU/AU) zilipambwa na shughuli mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kuwasha mwenge wa AU, maandamano na burudani kutoka
vikundi mbalimbali vya utamaduni. Aidha, sherehe hizo zilihudhuriwa na
Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimatafa hapa nchini, wanafunzi
na wananchi.