Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (katikati) akisindikizwa na
Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa, Bw. Raymond Mbilinyi
(kulia) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kitaifa wa Majadiliano kwa manufaa ya wote jana jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kitaifa wa Majadiliano kwa manufaa ya wote ulioanza jana jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali
imesema Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya wote yanalenga
kuwawezesha watanzania kumiliki uchumi wao na nchi kufikia uchumi wa
kati kufikia mwaka 2025.
Akiongea
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati wa siku ya pili
ya mkutano wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya wote Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu
alisema serikali imejipanga kuona majadiliano hayo yanaleta mapinduzi ya
kiuchumi na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi wa viwanda katika
eneo hili la Afrika.
“Serikali
imedhamiria kuhakikisha majadiliano haya yanaleta manufaa kwa wananchi
wake na majadiliano haya yanatoa msukumo wa kipekee kufanikisha hili,”
alisema.
Dkt. Nagu
ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo kwa niaba ya ya Makamu wa Rais,
Dkt. Ghalib Bilal alisema serikali inataka kuona takwimu za kukua kwa
uchumi wa nchi unaendana na maendeleo ya watu wake katika kila pembe ya
nchi na kwa kila mtu.
Mkutano
huu wa siku mbili uliomalizika jana ni matayarisho ya mkutano wa
kimataifa wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya wote au “Smart
Partnership Dialogue Global 2013” unaotarajiwa kufanyika mwezi Julai
mwaka huu hapa Tanzania.
Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kama taasisi ya serikali ilipewa jukumu la kuratibu majadiliano haya kitaifa.
Akiwasilisha
mada katika mkutano huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Bw.
Lucas Kusima alisema usalama wa nchi ni mtaji wa maendeleo hivyo kila
mtu hana budi kulinda usalama wa nchi ili kufikia maendeleo ya kweli.
“Kama
usalama haupo hakuna wawekezaji wala watalii watakaokuja,” alisema na
kuongeza kuwa usalama ni muhimu katika kukuza ushirikiano wa kimataifa.
Alisema
dalili za usalama kutoweka hapa nchini kama migogoro ya kidini,
kisiasa, kugombea ardhi kati ya wafugaji na wakulima haina budi
kutafutiwa suluhisho la kudumu kwa faida ya wananchi.
“Kuna
umuhimu wa vyombo vya usalama kushirikiana na wananchi kuimarisha
usalama wa taifa zima kama kweli tunataka majadiliano haya yalete
manufaa,” alisema.
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Saidi Mwema alisema wakati umefika wa
makundi mbalimbali nchini kuunda kamati za ulinzi katika maeneo yao ili
kujihakikishia usalama.
Akitoa
mfano alisema maeneo ya ibada kama makanisa, misikiti, maeneo ya kazi,
na majirani wanaweza kuunda kamati za ulinzi na jeshi la polisi liko
tayari kuwawezesha mbinu mbalimbali za ulinzi katika maeneo yao.
“Jeshi la polisi linahitaji sana ushirikiano wa karibu na wananchi ili kufikia malengo ya usalama,” alisema.
Awali akifungua mkutano huo, Dkt. Bilal alipendekeza majadiliano hayo kuanza kufanyika kila mwaka hapa nchini ili kuharakisha maendeleo.
Dkt.
Bilal alisema kwenye ngazi ya mikoa na wilaya majadiliano hayo
yafanyike kila mwaka wakitumia mabaraza yao ya biashara ngazi husika
kabla ya majadiliano ya kitaifa.
“Mabaraza
ya biashara ya mikoa na wilaya yatasimamia utekelezaji wa mambo
yaliyokubalika ngazi husika na kufanyiwa tathmini kila mwaka,” alisema.
Makamu
wa Rais alisema kuwa majadiliano haya yanatoa fursa kwa viongozi wa
serikali kukutana na kada mbalimba za wananchi ili kujadiliana na
kuelewa mambo yanayochangia upatikanaji maendeleo endelevu.
Alieleza
kuwa uzoefu unaonesha kuwa, mtu mmoja mmoja au makundi ya watu,
wakishirikishwa na kuhamasishwa katika jambo lolote, na wakiliamini na
kulikubali; utekelezaji wake huwa rahisi.
“Azma
hii itatusaidia katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo ya
miakamitano na dira ya maendeleo ya taifa ya 2025,” alisema.
Alitaja
misingi ya majadiliano ambayo huleta maendeleo endelevu kama kuamini
kwamba jirani wa mtu akiendelea basin a watu wote wanaendelea na kwamba
maendeleo hayaji kwa kukwamishana na kulumbana bali kwa kushirikiana.
Alitaja msingi mwingine kuwa ni watu wote ni sawa bila kujali nyadhifa zao kwenye jumuia wanazoishi.
“Kila mtu anao mchango mkubwa katika kuleta maendeleo katika jumuiya anayoishi,” alisema.
Alisema
kuna umuhimu wa kuachana na dhana potofu ambayo viongozi wa juu hutoa
maagizo ngazi ya chini kwa utekelezaji na kuwa viongozi wakubali kupokea
na kuthamini ushauri toka chini kwenda juu kwa utekelezaji.
Alitaja msingi mwingine kama ni kuwa na muono wa pamoja na utekelezaji wa nidhamu wa hali ya juu.
Kabla ya majadiliano haya TNBC iliendesha mikutano ya kuelimisha wananchi kupitia makundi mbalimbali kupitia katika jumla ya kanda 11; tisa Tanzania bara na mbili Tanzania visiwani mmoja Pemba na mwingine Unguja.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na watu zaidi ya 500 wakiwemo viongozi wa serikali
toka mikoa yote, vikundi mbalimbali na sekta binafsi.