Monday, June 10, 2013

TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA TGNP

Bi UsuMallya 
MkurugenziMtendaji 


Mrejesho wa  utafiti shirikishi wa uraghbishi -Kata za Mshewe – Mbeya vijijini,  Kisaki- Morogoro vijijini; na  Kishapu - Shinyanga

TGNP Mtandao ni Asasi  inayotetea na kuweka chachu katika harakati za ujenzi wa jamii yenye kuzingatia haki za wanawake , usawa wa kijinsia na haki za kijamii katika ngazi zote. Tangu kuanzishwa kwake, TGNP Mtandao imekuwa inatumia Uraghbishi na  Ushiriki kama mbinu muhimu za kujifunza,

 kutafakari, kuchambua na kutekeleza mikakati mbalimbali ya ujenzi wa Tapo la ukombozi wa wanawake kimapinduzi lililokita katika  ngazi ya msingi ya kijamii na lenye uwezo kwa kudai uwajibikaji katika kutoa huduma bora , kusimamia rasilimali za taifa  ili ziwanufaishe makundi yaliyoko pembezoni hususan wanawake. 

Lengo kuu ni  kujenga mifumo mbadala dhidi ya mfumo dume , uliberali mamboleo na mifumo yote kandamizi[1]. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuendeleza kampeni ya Haki ya Uchumi: Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake Walioko Pembezoni ambayo imewezesha kujenga nguvu za pamoja na kuongeza uelewa wa masuala ya kijinsia na ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi mbalimbali hapa nchini na hata nje ya nchi. 

Kutokana na juhudi hizi,  Mwezi Mei 2013, kikosi cha waraghbishi[2] toka TGNP kiliwezesha  utafiti shirikishi katika Kata  za Kishapu (Shinyanga) ;Mshewe( Mbeya vijijini) na Kisaki ( Morogoro Vijijini). Utafiti huu ulikuwa ni mwendelezo wa Utafiti kama huu uliofanyika mwaka jana katika Wilaya husika. 

Kwa mwaka huu utafiti ulifanyika katika vijiji 14 kwenye maeneo yote..  Waraghbishi ngazi ya jamii walitoa mrejesho kwa viongozi wa Vijiji, kata na Halmashauri na kuwasilisha changamoto zinazozikabili kata hizo hususan katika masuala ya  huduma bora za kijamii, kunufaika na rasilimali, haki za wanawake  na za kijamii. Utafiti huu ulifuatiwa na  warsha za kuanzisha vituo vya taarifa na maarifa, na ya waandishi wa habari na habari za kiuchunguzi.

Lengo kuu  la uraghbishi na utafiti shirikishi lilikuwa ni kuwezesha ushiriki wa wanawake, wanaume, makundi na mitandao  katika ngazi ya jamii  kufanya   uchambuzi wa hali halisi kwa mrengo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi ; kuibua kero na changamoto zinazokabili makundi husika na za pamoja ; Mchakato huu pia ulilenga katika kukuza uwezo na uelewa wa  uchambuzi wa kero zinazoikabili jamii  na jinsi zinavyofungamana  na mifumo kandamizi kama  utandawazi wizi/uliberali mamboleo, mfumo dume, mila, desturi, sera mbovu na jinsi zinavyosababisha mgawanyo mbaya  wa rasilimali za taifa.  Muhimu pia ilikuwa ni  kujenga nguvu za pamoja katika kudai  na kushiriki katika  kupanga mikakati ya kutatua kero hizo.

A: Masuala  makuu yaliyojitokeza katika Utafiti shirikishi na uraghbishi:
1.      Changamoto za uwekezaji na  mgawanyo  mbaya wa ardhi kwa wananchi hususan Kata ya Mshewe Mbeya Vijijini.
Utafiti ulibani  kuchukuliwa kwa , kwa maeneo ya ardhi katika kijiji cha Mshewe – Mbeya vijijini  yenye rutuba hali inayosababisha wananchi kukosa maeneo ya kutosha kwa ajili ya kilimo na makazi; na hivyo.

 kulazimika kuwa vibarua katika mashamba ya wawekezaji  ili waweze kijikimu kimaisha na wanaume kulazimika kutoa rushwa ya pesa ili kupata kazi katika mashamba hayo. 

Wanawake na wasichana wamekuwa wakifanya vibarua katika mashamba ya wawekezaji kwa ujira mdogo kati ya shilingi (2,500/- na 3000/- tu kwa siku).Wakati huo huo  wanakumbana na ukatili katika ajira hiyo ikiwemo rushwa ya ngono, hali ambayo inasababisha  ongezeko la  magonjwa ambukizi yakiwemo VVU na Ukimwi.

 Katika Kata ya Kisaki, Morogoro Vijijini  mgogoro mkubwa wa ardhi ni kati ya  wakulima wadogo wadogo na wafugaji, unaosababisha kuharibiwa kwa   mazao ya wakulima  kutokana na kukosekana kwa eneo la wafugaji. Migogoro hii imezaa tatizo la rushwa, ambapo wafugaji wanadaiwa kuhonga viongozi ili wasisumbuliwe wanapoingilia maeneo ya wakulima.

2.      Upatikanaji wa  maji  safi na salama
Pamoja na Sera ya Taifa ya Maji kuweka lengo la kupatikana kwa maji katika umbali kwa mita 400;  bado maji safi na salama ni changamoto kubwa kwa wakazi wa Kishapu na Mshewe    linalotishia maisha  na afya zao.  


  Mfano katika kijiji cha Ilota- Mshewe, licha ya uhaba mkubwa wa maji wananchi wanasaka  maji katika eneo hatarishi huku wakichangia maji kidogo yasiyo safi wala salama pamoja na mifugo. Cha kusikitisha  wananchi hawa wamechanga pesa  kwa ajili ya maji kwa muda mrefu bila mafanikio.

 Katika vijiji vya Isoso na Lubaga Kata ya Kishapu,  hali ya ukosefu wa  maji,  inasababisha wanawake na wasichana kutembea umbali mrefu na kujikita katika mazingira hatarishi ambayo  yamesababisha ongezeko la mimba za utotoni,  ubakaji kwa wanawake na wasichana na  vipigo . 

Tatizo hili  limeongeza umasikini wa kipato kutokana kutumia muda mwingi na rasilimali kusaka maji. Kilio chao kikubwa ni kupata vyanzo mbadala vya maji hasa kutoka zi wa Victoria.
3.      Ukosefu wa huduma bora za afya:
Utafiti uliibua changamoto kubwa katika maeneo yafuatayo

3.1       Kijiji cha Ilota, Mbeya Vijijini wananchi wamekiri kutokuwepo na  zahanati hali inayosababisha wanawake wajawazito kujifungulia majumbani. Kati ya wanawake 20 waliohojiwa ni mmoja (1) tu ambae alishawahi kujifungua katika hospitali ya Mbalizi . Wengi  wamekiri kujifungulia kwa wakunga wa jadi kwa kukosa fedha za kutosha kwa ajili ya kwenda hospitali zilizoko mbali na kijiji.

3.2.Kata ya Kisaki Morogoro vijijini, tatizo kubwa ni ukosefu wa dawa na wahudumu wa afya katika zahanati za vijiji vya Gomero, Station na Nyarutanga ambapo kuna majengo mazuri bila wahudumu, dawa wala vifaa tiba kwa ajili ya uchunguzi.  Vile vile wananchi wanachangia  gharama kubwa usafiri wa gari ya wagonjwa   shilingi. 70,000/= kwenda Morogoro hususan wanawake wanaokwenda kujifungua. Daktari wa Kituo cha afya, Kisaki alikiri  kuwa tangu Oktoba 2012 hawajapokea dawa wala kifaa tiba chochote kutoka Stoo ya Madawa ya serikali (MSD) hali inayosababisha wanawake wengi kukosa huduma, na wengine kupata ulemavu wa kudumu na hususan fistula

4.      Uongozi mbovu na Rushwa
Suala la viongozi kutowajibika lilijitokeza kama suala mtambuka pamoja na suala la rushwa katika maeneo yote. Haya yalielezwa kuwa kiini cha changamoto zilizojitokeza, ukosefu ,wa huduma za msingi kwa wanawake na wanaume walioko pembezoni. 


Vile vile kuwepo na usiri wa taarifa za mapato na matumizi, , viongozi kutowashirikisha wananchi katika masuala ya maendeleo,viongozi ngazi za vijiji kuruhusu video za ngono viongozi kutotekeleza ahadi zao kwa wananchi.

5.      Unyanyasaji wa wanawake na wasichana  
Unyanyasaji wa kijinsia umejitokeza kama suala mtambuka  katika maeneo yote. Mfano  tatizo la maji linasababisha vipigo kwa wanawake, ubakaji, elimu duni kwa wasichana, mimba za utotoni na ukosefu wa kipato. Kwa upande wa uwekezaji/ ardhi, wanawake  na wasichana wamekumbana na rushwa ya ngono, ajira isiyo na staha pamoja na kipato kidogo na kwa upande wa afya, wanawake wamekuwa wakidaiwa fedha na vifaa  wakati wa kujifungua   na hata kujifungulia  katika mazingira hatarishi.

B:        Masuala makuu ya kufuatilia

1          Katika Serikali na Uongozi  Serikali za Mitaa( Vijiji, kata na wilaya)  na Serikali Kuu
  • Serikali  irejeshe ardhi  ya Kata ya Mshewe inayomilikiwa na wawekezaji wa nje na ndani ya nchi, kwa manufaa ya wananchi sasa na vizazi vijavyo. 

  •  Pia Serikali itenge maeeneo la wafugaji kata ya Kisaki na kuboresha ulinzi dhidi ya wanyama wanaoharibu mazao na wananchi walioathirika na migogoro ya wakulima na wafugaji walipwe fidia.
  • Viongozi wasitumie changamoto za wananchi kisiasa hususan wakati wa kampeni za uchaguzi. Kwa mantiki hii viongozi waliowaahidi wananchi wa  kata ya Kishapu kuhusu  upatikanaji wa maji watimize ahadi zao mara moja.

  • Serikali iboreshe mfumo wa  utoaji wa pembejeo ziwe za kutosha na ziwafikie wakulima wadogo wadogo kwa wakati muafaka. Pia  kuwepo na maeneo ya masoko kwa ajili ya kuuza mazao ya wakulima.

  • Huduma za afya katika kata ya Mshewe, Kisaki na Kishapu  ziboreshwe  hasa katika upatikanaji wa dawa, vifaa na wahudumu. Kwa   kijiji cha Ilota , Serikali itenge bajeti kwa ajili ya ujenzi wa zahanati.  Pia tunasisitiza kuwa wahudumu wa afya wanaodai  wajawazito na wazee pesa  waache mara moja hii ni pamoja na magari ya wagonjwa  yanayodai wajawazito pesa kata Kisaki

  • Kuwepo na mfumo wa kuwawajibisha viongozi wote wanaokiuka maadili ya kazi zao ili kuondokana na aina zote za rushwa na ukatili wa kijinsia hasa ukatili kwa wanawake na wasichana. Mfano viongozi wanaoruhusu video za ngono hadharani hasa kata ya Mshewe  waache mara moja.

2          Viongozi wawakilishi hususan madiwani na wabunge
Kutumia matokeo ya utafiti kudai uwajibikaji wa serikali kwa wananchi katika ngazi zote kupitia bajeti, ripoti ya mkaguzi mkuu wa serikali, kudai sera ya haki ya uhuru kwa wananchi na mikakati mbali mbali ya maendeleo.
3          Taasisi za kitafiti, makundi ya Kiraia na Vyombo vya Habari
  • Kutumia uraghbishi kama mbinu ya kuibua masuala ya wanajamii na kujenga uwezo wa wanajamii kuhoji na kudai uwajibikaji
  • Kuendeleza harakati za ukombozi ws wanawake kimapinduzi katika ngazi zote za maamuzi ikiwemo kitaifa, kikanda na kimataifa kw mfano kupitia mchakato wa kujenga malengo mapya ya Millenia ya 2015.

Limetolewa na:

UsuMallya 
MkurugenziMtendaji 
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)