Na Anna Nkinda – Yokohama
Imeelezwa
kwamba inawezekana kuwa na kizazi kipya barani Afrika kisichokuwa na
maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kama jamii nzima itaamua kupambana na
ugonjwa huo unaosababisha vifo vya watu wengi hasa kina mama wajawazito
na watoto.
Hayo
yamesemwa leo na Mke wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) mama Ban
Soon –taek wakati akifungua kongamano la kimataifa la siku mbili la
Tuongee kuhusu Ukimwi : Afrika na Japani tushirikiane kutatua
changamoto unaofanyika mjini Yokohama.
Mama
Ban Soon alisema kuwa ni wajibu wa wake wa marais wa Afrika
kuhakikisha kuwa hakuna maambukizi mapya yaUkimwi, unyanyapaa na vifo
vya watoto chini ya umri wa miaka mitano katika nchi zao.
Jambo
ambalo siyo rahisi kwa nchi maskini kwani kila siku watoto mia tisa
wanapata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) , kama hali hii
itaendelea watoto zaidi ya milioni watakuwa wamepata maambukizi ifikapo
mwaka 2015.
Alisema
kuwa nia ni kuwafikia wanawake wajawazito wote wanaohitaji kuangaliwa
na kupewa matibabu hii inawezekana kama watashirikiana kwa pamoja na
hivvyo kuzaliwa watoto wasio na maambukizi na baada ya miaka michache
hakutakuwa na ugonjwa wa Ukimwi barani Afrika.
“Kama
itatokea mama mjamzito anaugonjwa wa Ukimwi basi ajifungue salama bila
ya kumuambukiza mtoto wake, pia amtunze mtoto huyo kwani ni wajibu
wetu kuwalinda mama na mtoto wa bara la Afrika”, alisema Mama Ban Soon.
Akiwakaribisha
wake hao wa marais katika mkutano huo mke wa waziri mkuu wa Japani Mama
Akie Abe alisema kuwa wanawake na watoto wote Duniani wanapambana na
matatizo yanayofanana ingawa ukubwa wa matatizo unatofautiana hivyo basi
wao kama viongozi wanatakiwa kuungana kwa pamoja na kuwasaidia wanawake
hao.
Mama
Abe alisema, “Hapa nchini Japani idadi ya watu wanaoishi na VVU inazidi
kuongezeka na Serikali inawapatia huduma mbalimbali, lakini wanawake
wengi Duniani wanaogopa kuongea kuhusu ugonjwa wa Ukimwi, wakati umefika
sasa wasiogope waongee ili waweze kupata haki zao za msingi”
Kwa
upande wake Rais wa Umoja wa wake wa Marais wa Afrika wa kupambana na
Ugonjwa wa Ukimwi (OAFLA) Mama Penehupifo Pohamba aliishukuru Serikali
ya Japan kwa kuandaa mkutano huo na kutoa zaidi ya dola bilioni moja za
Kimarekani barani Afrika kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya Ukimwi,
Maralia na kifua kikuu.
Alisema
kuwa ni jambo la muhimu kuweka ushirikiano wa pamoja baina ya Afrika
na Japani na kuwaomba wasaidiwe rasilimali fedha ambazo zitawasaidia
kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wanawake na watoto.
“Wanawake
wengi na watoto wanakufa na ugonjwa huu hii ni kutokana na baadhi ya
mila zinazowakandamiza katika jamii zao pia baadhi ya nchi zetu
zinakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe jambo la muhimu ni kuungana
kwa pamoja ili tuweze kuwasaidia na kutimiza malengo yetu”, alisema
mama Pohamba.
Baadhi
ya wasomi na wataalamu mbalimbali waliowasilisha mada katika mkutano
huo waliwaomba wake hao wa Marais kupaza sauti zao kwa pamoja na
kuwasaidia watu wanaoishi na VVU hasa kina mama na watoto ambao hawana
mahali pa kusemea matatizo yao.
Walisema
kuwa tatizo la unyanyapaa ni kubwa sana Barani Afrika hivyo basi
wanatakiwa kuielimisha jamii inayowazunguka ili iweze kutambuwa kuwa
ugonjwa Wa UKimwi ni sawa na magonjwa mengine na kutowatenga watu wenye
VVU.
“Wasomi
peke yao hawawezi kukabiliana na tatizo la Ukimwi bali jamii nzima
inatakiwa kuungana kwa pamoja kutatua changamoto hii, hali hiyo
itapunguza unyanyapaa miongoni mwa jamii inayotuzunguka”, alisema Dk.
Peter Piot kwa niaba ya wenzake.
Wakitoa
mawazo yao wake hao wa marais waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa
licha ya ugonjwa wa UKimwi kuua watu wengi Barani Afrika pia kuna
ugonjwa wa kansa ya Shingo ya kizazi, matatizo ya uzazi hasa wakati wa
kujifungua ambayo yanaua wanawake na watoto wengi na unyanyasaji wa
kijinsia.
Nao
baadhi ya wanawake wanaoishi na VVU kutoka barani Afrika waliuomba
umoja huo uweze kuwasaidia kwani bado kuna unyanyapaa mkubwa hasa kwa
wanawake na watoto katika jamii inayowazunguka.
Kongamano
hilo ambalo kwa mara ya kwanza limehudhuliwa na wake wa marais wa
Afrika akiwemo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye kupitia taasisi
yake ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) anafanya kazi ya kuhakikisha kuwa
tatizo la vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua nchini,
kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuhakikisha kuwa mtoto wa kike ambaye
ni yatima na anatoka katika mazingira hatarishi anapata elimu sawa na
watoto wengine.
Wizara
ya mambo ya Nje ya Japani ndiyo iliyoandaa Kongamano hilo kwa
kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha Japani cha mabadilishano na
mradi maalum wa wanafunzi kwa ajili ya Mkutano wa tano wa kimataifa wa
Tokyo kwa maendeleo ya Afrika (TICAD).