Maparachichi yanayouzwa na SACOMA toka Kenya
Kutoka
Kulia Bw. Nigel Shepherd, Mh. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Bi. Perez
Ochieng, Balozi Peter Kallaghe. Waliosimama nyuma, Bw. Sam Ochieng
(SACOMA), Bw. Hugh Morris na Bw David Smith
Mh. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na
msafara wake wakiondoka eneo la ghala la soko kuelekea mkutanoni. Kulia
kwake ni Balozi Peter Kallaghe na Mkurugenzi wa SACOMA, Sam Ochieng.
--
CHANGAMOTO : UWEZEKANO WA
WAKULIMA, VIJANA NA WAFANYABIASHARA KUUZA BIDHAA UINGEREZA
Imeandikwa kwa ushirikiano wa Urban Pulse na Freddy Macha
--
Ijumaa iliyopita itajulikana kama siku mlango mdogo ila muhimu sana
ulipofungua kitasa chake kwa baadhi ya wananchi wanaojituma kikazi na
kibiashara Tanzania. Waziri Mkuu,
Mheshimiwa Mizengo Pinda alitembelea soko la mboga na matunda lililoko
Leytonstone, mashariki ya London.
Matembezi yalidhihirisha mahusiano ya ujirani
mwema kati yetu Watanzania na Kenya yenye kampuni iliyoshajijenga ndani ya soko hili
maarufu na kubwa sana.
Soko hilo linaloitwa Spitalfields si
sehemu inayofahamika na wengi wanaoishi
Uingereza licha ya kwamba jina hilo si rahisi kutamka au kuandikwa. Lakini Spitalfields (tamka “Spitol-fildz”),
itakua eneo muhimu sana kwa vijana, wakulima
na wafanyabiashara Tanzania, miaka ijayo.
Hapa
ndipo mboga na matunda toka sehemu mbalimbali duniani huletwa halafu
zikasambazwa maduka makubwa ya vyakula Uingereza. Hivyo
basi mlango kufunguliwa ni “uwanja muafaka”
kwa wote wanaojituma na kutaka maendeleo kiuchumi.
Spitalfields ina zaidi ya miaka mia tatu. Ingawa ilipoanzishwa makao yake yalikuwa mtaa wa Brick Lane karibu na Liverpool
Street, leo tawi jipya, New Spitalfields
Market limehamishwa karibu uwanja yalipofanyika mashindano ya Olimpiki mwaka
jana. Tawi hili lilifunguliwa rasmi 1991 na linaongoza Ulaya nzima kwa usambazaji wa
matunda na mboga toka nchi zenye joto duniani.
Kati ya nchi hizo ni ndugu zetu wa
Kenya kupitia kampuni yaSACOMA(“Sahara Communities Abroad”) iliyoanzishwa mwaka 2000 kuendeleza wananchi
wasiojiweza kiuchumi na kielimu walioko jimbo la kusini ya jangwa la Sahara
wanaozungumza Kiswahili. Licha ya kusafirisha bidhaa na kuziuza New Spitalfields, SACOMA , anasema msemaji
wake Bi Perez Ochieng hutoa ajira kwa takriban watu 30,000 Ulaya na Kenya.
Perez Ochieng, mumewe Sam Ochieng (mkurugenzi SACOMA) na meneja mwendeshaji
New Spitalfields, Bw. Nigel Shepherd
walimtembeza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiongozana na Balozi wetu Ungereza , Mhe
Peter Kallaghe, mkurugenzi wa Kituo cha Biashara Tanzania, London, Yusufu
Kashangwa na maofisa wengine. Ubalozi wa
Tanzania Uingereza ndiyo ulioratibu na kuandaa tukio zima.
Waziri Mkuu na wenzake
walikuja London kuhudhuria mkutano wa kimataifa unaoangalia namna ya kuondoa
njaa na umuhimu wa lishe bora kwa kina mama na watoto ulimwenguni. Mkutano umeandaliwa na asasi za serikali na zisizo za
kiserikali kukutanisha mataifa makubwa (yaani G8), wachangiaji, wadhamini na watoaji misaada kwa
lengo la kutokomeza njaa na kusaidia kuwapatia kina mama na watoto lishe bora.
Baada ya matembezi ndani ya ghala, SACOMA iliandaa kikao kifupi kuonyesha namna na pia mazao gani
huuzwa. Baadhi ya mazao yaliyowekwa
mezani kilipofanyika kikao ni pamoja na mahindi ya kuchemsha, ndizi kisukari, juisi za
matunda, viazi vitamu, maembe sindano na mboga maarufu ya Sukumawiki ambayo
hutumiwa zaidi Kenya. Sukuma Wiki (iliyo ndani ya familia ya mboga za kabeji)
huuzwa tayari imefungwa kwenye mifuko na SACOMA.
Wakati wa kikao hicho wazungumzaji wahusika walieleza namna ambavyo soko
litawafaidi wakulima , vijana na wafanyabiashara wa Tanzania hasa wale
wanaojituma.
Meneja Mwangalizi wa soko, Nigel Shepherd
na Wana SACOMA walifafanua baadhi ya masharti yanayotakiwa kufikiwa kuleta
bidhaa hizi sokoni. Mojawapo ni kuzingatia taratibu za uuzaji wa mazao
uliowekwa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU). Taratibu hizo ni mathalan upandaji
mazao unavyofanywa kusudi umudu safari ya muda mrefu, hifadhi yake katika
makasha ya baridi, usafi wa jumla, ufungaji na utangazaji (branding).
Perez Ochieng alitoa mfano namna
SACOMA ilivyojitahidi kuwahusisha vijana wa Kenya katika kilimo ambacho
kimewaletea ajira na kuboresha maisha
yao. Akifafanua Perez alisema kawaida vijana waishio mijini huwa hawavutiwi na kazi za
kilimo lakini kuna “mengi ya kuzingatiwa ikiwemo kazi za kupakia bidhaa,
kuzifunga katika mifuko, uendeshaji magari, uandishi wa makasha, nk.”
Akiendeleza hoja zaidi Waziri Mkuu ambaye kazaliwa mazingira ya kilimo
alisema shughuli hii imedunishwa na mtazamo kuwa ni kazi ngumu na chafu ya
jembe tu. “Inabidi tuweke mazingira yatakayowafanya
vijana waone kazi zao zinaweza kupata soko. Kazi kubwa inahitajika kufanywa
kuwafanya vijana wapende kilimo.”
Akitoa mfano wa kampuni ndogo ya vijana wa Gongo Seke walioamua kufanya
biashara ya kilimo cha bustani
aliyotembelea karibuni mkoa wa Mwanza, Waziri Mkuu alisema hiyo inathibitisha wapo
wanaoweza kufuata fani hii.
Mheshimiwa Pinda aliwahakikishia wenyeji kwamba si tatizo hata kidogo kwa
Tanzania kuuza bidhaa zake.
Akithibitisha uzoefu wake kama mkulima, Waziri Mkuu aliwachekesha
wasikilizaji aliposhika moja ya ndizi
kisukari zilizokua mezani akasema Watanzania wanaweza kuleta ndizi zilizovimba
zaidi na maembe dodo makubwa kuliko yale sindano yaliyoonyeshwa.
Kufuatana na takwimu zilizotolewa na idara ya habari ya CNN mwaka jana,
ingawa uchumi wa Afrika unatazamiwa kukua kwa asilimia 4.5 idadi
ya vijana inatazamiwa kuongezeka mara mbili barani mwaka 2045. Leo
asilimia 30 ya vijana walio na umri kati ya miaka 18 hadi 29 hawana ajira
katika jamii nyingi za Afrika.