Ndugu zangu,
Nimerejea tena kwa jambo hili la Kitaaluma,
Kabla ya kuandika tahariri yangu ya leo naomba kuwaalika wadau kuwa na mawazo huru juu ya hili nitakaloandika. Nasema hivyo kwa sababu nikiwa mwandishi wa habari naamini katika uhariri.
Mjadala kuhusu Mgongano wa kimaslai bado ni somo pana kwa waandishi wa Habari, ni somo linalohitaji kukumbushana kila uchao, ni somo ambalo hata wadau wa waandishi wa habari wanapaswa kulijua na kama hawajui waelekezwe na ni somo ambalo wanajamii ambao ndio tunaowahudumia wana haki ya kulijua.
Kwa kifupi Mgongano wa kimaslai kwa mwandishi wa Habari ni pale shughuli anazofanya au anazotarajia kuzifanya kwa maslai ya umma zinapoathiriwa ama kuathiri maslai yake binafsi.
Kwa Mfano, Mwandishi wa Habari za Uchunguzi kuhusu kuvuja kwa gesi katika kiwanda kunakochafua mazingira ilihali yeye mwenyewe ni msambazaji wa malighafi katika kiwanda hicho, kwa namna yoyote atakua katika mgongano wa maslai kwa sababu anaweza kuficha ukweli kuhusu athari za kiwanda hicho ili kulinda maslai ya biashara yake ya kusambaza malighafi katika kiwanda hicho.
Mfano mwingine ni wa Mwandishi wa Habari anayetaka kuandika habari kuhusu Njama za watendaji wa Halmashauri fulani wanaofuja fedha za wananchi ilihali ndani ya Halmashauri hiyo kuna Mjomba wake na ndio anayegharamia maisha yake kwa sehemu kubwa na hata kama hagharamii. Mwandishi huyu kwa namna yoyote hawezi kuandika kikamilifu tatizo hilo kwa kuhofia kumuumiza mjomba wake.
Lakini katika kazi hii ya uandishi wa habari ipo Mifano mingi ambayo inaigusa zaidi fani hii na ambayo kwa kweli inatuondolea uaminifu mbele ya jamii.
Sio nia yangu kudai migongano ya Maslai ikome leo lakini nia yangu tukumbushane tu wale tulio katika migongano hii, tuwe tunajua kwamba tuna kazi ya kuondokana na migongano ya kimaslai.
Matharani tupo tulianzisha uswahiba na wadau ambao kimsingi uswahiba wetu unasababisha mgongano wa kimaslai katika kazi yetu, tupo tuliajiriwa katika taasisi, kampuni na wafanyabiashara ambako kimsingi mgongano wa maslai katika kazi ya kuihudumia jamii hauepukiki.
Lakini leo naandika haya nikiwa na lengo la kuwaalika waandishi wa habari tuamue kuanza safari ya kuepuka migongano ya kimaslai. Itatusaidia kuaminika katika jamii, itatusaidia kuwa huru katika kuandika habari, itatusaidia kuandika habari zenye tija katika jamii na pia itatupa heshima japo najua safari hii ni ngumu na nzito kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo uchumi (maslai duni) nakadharika
Hata hivyo yapo maeneo ambayo mimi nadhani tunaweza kuanza kwa mfano, vyombo vyetu vikubwa vinavyotuunganisha kama vile Press Clubs, UTPC, MCT, TEF nakadharika vianze kuepuka mianya ya mgongano wa maslai kama vile uswahiba na Wamiliki wa vyombo vya habari, kuepuka misaada ya wafanyabiashara na watu wengine ambao mwisho wa siku wanasababisha migongano ya kimaslai, waliomo katika vyombo hivyo (watendaji na viongozi) wawe watu huru na hata tukikutana nao barabarani tuwaone wakiwa huru.
Zaidi ya hapo vyombo hivi kwa sasa naamini vinapata mchango mkubwa kutoka kwa wafadhili vianze kufikiria njia za kutoendeshwa kwa ufadhili. Kwa sababu haina ubishi hata mtoto humuheshimu na kumlilia ampaye maziwa kila siku.
Halafu hata wale wadau wetu wanaotufadhili katika habari za uchunguzi waangalie upya utaratibu wao wa kututaka tupeleke kwanza proposal ya kile tunachotaka kuchunguza ndipo tupatiwe fedha za kwenda kutekeleza uchunguzi wetu. Mimi hujiuliza hivi nikipekeleka proposal ya kumchunguza mjomba wa anayepitisha hiyo proposal ambaye nina taarifa kuwa ana mradi wa majambazi, proposal yangu itapita? Na ikipita nitakua salama? Au ndio kung'oana kucha na kutobolewa macho? Its a challenge.
Tuzungumze, tusisubiri kuzungumziwa. Tukizungumza tuchukue hatua. Tusikate tamaa kwa kuwa Jamii inatutegemea
Mwisho naomba sote tuunge mkono kauli mbiu ya "Trust Me I'm a Journalist" kwa kiswahili "Niamini mimi ni mwandishi wa Habari"