Saturday, June 1, 2013

TUJADILI; Hivi ni sawa kuiba mataji yanayowekwa kwenye makaburi?

Tahariri ya Gerson Msigwa

Jamani !!!!!!!!!!!!
Hivi karibuni nimeshiriki Msiba wa dada mmoja au niseme Shemeji yangu, yaani mke wa rafiki yangu. Nilijiuliza maswali mengi baada ya shughuli ya kuuzika mwili wa Marehemu kumalizika, ndugu waliojawa na majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao wanalazimika kuzima majonzi yao na kuanza kwa pamoja kuyachoma mataji ya maua waliyoyapamba katika kaburi la mpendwa wao kwa hofu kuwa mara watakapoondoka mataji hayo yataibiwa na imekua hivyo. Kwa hiyo yanachomwachomwa ili yasiweze kurudishwa dukani tena.

Sasa kwa tukio hili na mengine mengi yanayofanyika katika maziko ambayo nimepata kuyashuhudia nikajiuliza maswali hivi Watanzani tumefika mahali tunavizia kupata kipato kisicho halali hata katika matukio ya majonzi kama haya ya vifo? Nikajiuliza tumetokwa na utu au ni changamoto za ugumu wa maisha? Nikajiuliza mbona mambo haya hayakutokea zamani? Nikajiuliza kama hakuna huruma katika matukio kama hili tupo salama kwenye lipi? Nikajiuliza kama tunashindwa kuwa wavumilivu kwenye tukio kama hili tunaweza kuwa wavumilivu kwenye rasuilimali za nchi?

Hata hivyo nikajikuta nakaribia kupata majibu kwa nini nchi inateketea, kwa nini Taifa halijengwi na kwa nini upendo hakuna na kilichobaki ni kuviziana.

Mkulima anamvizia mnunuzi wa mazao yake, Mnunuzi anamvizia Mkulina, Mfanyabiashara halikadharika, Viongozi nao wanawavizia wanaowaongoza na wanaoongozwa wanawavizia viongozi wao, wenye madaraka wanawavizia wasio na madaraka na wasio na madaraka wanawavizia wenye madaraka.

Hapo unaweza kusema mengi lakini kwa kifupi, TUMEKUA TAIFA LA KUVIZIA, TENA KWA MADAI KUWA TUNATUMIA BONGO.

Nimalizie kwa swali la Mkongwe Makwaiya wa Kuhenga- JE TUTAFIKA?


Pichani; Ndugu wa Marehemu wakipamba Kaburi la Mpendwa wao baada ya kukamilika kwa zoezi la maziko katika maburi ya Songambele Mjini Songea.


Mara zoezi la kuchoma maua linaanza, na hapo hakuna ua wala taji linaloachwa bila kuguswa na moto.