Umewahi
kuingia ndani ya Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo? Binafsi kwa mara ya
kwanza niliingia Jumatano iliyopita, nikifuatilia kesi, kama
ijulikanavyo kazi za waandishi wa habari. Nikiwa
ndani ya ukumbi wa mahakama ya wazi, sikuamini nilichokishuhudia katika
mji huo maarufu wa kihistoria, kitaifa na kimataifa; ikiwa ni pamoja na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kuwa mzaliwa wa
wilaya hiyo.
Hata Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa ni mbunge wa jimbo hilo lenye vivutio vingi vya kihistoria.
Macho yangu
yakatua katika paa la mahakama hiyo na kupokelewa na mabati
yaliyotoboka-toboka, ilhali nyaya za umeme zikiwa zimetandazwa kupitia
baadhi ya nguzo kwa minajili ya kusambaza umeme ndani ya jengo hilo.
Nikarejesha
fikra zangu kwenye tukio la kuporomoka jengo lililokuwa na ghorofa 16
hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Nikaanza kuingiwa hofu kutokana na
baadhi ya kuta kusheheni viraka huku nyufa nyingine zikishindikana
kudhibitiwa na viraka, hali iliyosababisha kuta kuwa na michirizi na
hivyo kutoa taswira ya uchakavu wa jengo hilo.
Nikabadili
uelekeo. Nikayaelekeza macho upande wa kushoto kwangu, pembezoni mwa
vizimba, jirani na mlango unaotumiwa na hakimu kuingia mahakamani.
Nikahisi kuishiwa nguvu baada ya kuona majalada yakiwa yamehifadhiwa
katika eneo lisilo na mlango wala dirisha.
Panapotakiwa
kuwa na dirisha, pamewekwa mbao laini na kufunikwa kwa mapazia.
Ikumbukwe hata kama majalada hayo ni ya kesi zilizoisha, haimaanishi
kumbukumbu zake hazina maana.
Nikainamisha
uso nikiwaza jinsi ya kutumia kalamu yangu angalau kutimiza wajibu
wangu juu ya suala hili, macho yangu yakakutana na sakafu iliyochoka,
ikiwa na nyufa za kutosha.
Kwa mujibu
wa Katiba ya nchi, mahakama ni muhimili wa dola ambao ngazi yake ya
wilaya ina hadhi ya kupokea kesi za mauaji yaliyo kwenye hatua za
awali, wakili kutekeleza baadhi ya majukumu yao kushughulikia mashauri
ya madai, yenye thamani ya kuanzia Sh10 mil mpaka Sh100mil.
Katika hali
ya kawaida, ilitarajiwa jengo linalotumika kwa shughuli za mahakama,
liwe na hadhi inayoshabihiana na umuhimu, unyeti na usiri wake achilia
mbali hadhi ya utu wa mtumishi wa umma.
Kwanini hali inakuwa hivi?
Gazeti hili
lililazimika kuhojiana na uongozi kwa lengo la kujua kulikoni.Hakimu
Mfawidhi wa mahakama hiyo, Liad Chamshama anasema “Mahakama imekuwa moja
ya waathirika wa mfumo wa mgawanyo wa rasirimali za nchi usiozingatia
usawa, ukiwa makini utabaini serikali kuu inapendelewa zaidi ikifuatiwa
na wanasiasa.”
Anabainisha
kuwa ubovu wa jengo hilo nilioushuhudia si lolote, kwani hata Mhandisi
wa wilaya hiyo ameishasema tena kwa maandishi kuwa halifai tena kwa
matumizi.
Anasema
ilifika wakati wakalazimika kufanya ukarabati mdogo kwa kubadilisha miti
iliyoshika mabati kwenye paa wakaweka mbao, baada ya paa kuchakaa kiasi
cha kufanya waache kuendelea na kesi mvua zinaponyesha.
“Hata sasa
mvua ikinyesha inabidi niwaruhusu watumishi wakapumzike tu nyumbani
maana maji yanajaa eneo lote la mahakama, hapo nje kuna matofali
yamepangwa, mvua isipokuwa kubwa huwa tunayatumia kama njia ya kuingilia
mahakamani,”anafafanua Chamshama
Hata hivyo
anasema kwa kushirikiana na Mkuu wa wilaya hiyo, Ahmed Kiponzi
wanaendelea kujadiliana namna ya kujikwamua kutoka kwenye hali hiyo.
Anatoa wito
kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha kunakuwa na mgawanyo sawa wa
rasilimali, ili kuweka ufanisi mzuri katika uwajibikaji wa mahakama kwa
ujumla.
Akizungumza
na Mwananchi kwa njia ya simu, Kiponzi anakiri kuwa suala hilo ni nyeti
na lenye kuwafikirisha, kwamba atakapokutana ana kwa ana na gazeti hili
ataeleza mipango iliyopo.
Mbunge wa
jimbo hilo na waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa
anasema miongoni mwa mambo yanayomuumiza kichwa ni maboresho ya jengo
hilo la mahakama ya wilaya na kwamba jitihada zake zimekuwa zikikwama
kutokana na ufinyu wa bajeti ya wizara ya Sheria, Katiba na Utawala.
Kilo Khamis
Mdete (42) mkazi wa Bagamoyo anayejishughulisha na kilimo kijijini
Miono, akizungumzia hali ya mazingira ya mahakama hiyo ambapo alifika
kusikiliza kesi yake ya mgogoro na wafugaji, anasema:
“Siyo siri
hii ni aibu, mimi sikusoma ningekuwa nimesoma nina shahada yangu
nisingekubali kuletwa nifanye kazi kwenye ofisi kama hii. Hata mtu kutoa
rushwa ni rahisi kwa kuwa mazingira yanaashiria waliyomo wana njaa
kali.
Ofisi ikiwa
nzuri, mtu anakuwa na heshima na watumishi wanaofanyia kazi humo
wanaheshimika, hata wazo la kutoa rushwa likimjia mtu anahofu kwasababu
atajiuliza mara mbili atoe shilingi ngapi, hatimaye atahamasika kubaki
kwenye mstari wa sheria,” anasema Mdete.
Baadhi ya
wananchi wanalalamikia dharau za viongozi wakisema kuwa hawaoni umuhimu
wa kuboresha mahakama nchini, kwani zaidi ya majengo hata malipo mazuri
imekuwa ni tatizo.
Habari na Editha Majura
Chanzo - Mwananchi