Friday, April 12, 2013

BALOZI WA CHINA NCHINI AAHIDI KUSAIDIA KILIMO CHA MAHINDI SONGEA

  Naibu afisa uhamiaji wa mkoa wa Ruvuma Shaban  Omari akisalimiana na balozi wa China Nchini Tanzania Lu Younqing  mjini Songea 
 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea vijijini Rajabu Mtiula kushoto akimpa zawadi ya kinyago Balozi wa China
 Balozi wa China akikabidhi msaada wa Cherehani kwa katibu wa kikundi cha upendo Peramiho Leokadia Siwa
........................................................................................................................................
Na Nathan Mtega,Songea.

BALOZI wa china nchini Tanzania Lu Younqing ambaye yupo mkoani Ruvuma kwa ziara ya siku tatu ameahidi kuleta wawekezaji zaidi na watalaamu wengi katika sekta ya kilimo cha mahindi ili kulifanya zao hilo liwe  la kibiashara linalozalishwa kwa njia ya kilimo cha kisasa zaidi na kuwafanya wakulima wa zao hilo kujikwamua zaidi kichumi   .
 
Ahadi hiyo aliitoa wakati wa siku ya kwanza ya   ziara yake alipokuwa akikagua mashamba mbalimbali ya kilimo cha mahindi ambacho kinachofanywa na wakulima wa zao hilo latika jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma .
 
Katika ziara hiyo ya balozi Lu Younqing alitoa misaada mbalimbali kwenye vikundi vya kijamii na wakulima vilivyopo katika jimbo la Peramiho ikiwemo shule ya sekondari ya Namihoro iliyopo katika kijiji cha peramiho wilayani Songea mkoani Ruvuma.
 
Vikundi hivyo vilivyopata msaada huo ikiwemo  sekondari ya Namihoro iliyopewa shilingi milioni 10 ili kuendeleza elimu katika shule hiyo ,kikundi cha wakina mama wajasiriamali kilipewa  vyerehani 20 ili wajikwamue kiuchumi na baiskeli 20 kwa viongozi wa jumuiya ya vijana wa CCM wa kata zote za jimbo hilo la Peramiho.
 
 Aidha balozi huyo kabla ya kuhitimisha ziara yake hiyo ya siku tatu atatembelea pia mashamba ya kilimo cha kahawa yaliyopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ili kubaini changamoto zinazokabili kilimo hicho na kuwa akielekea wilaya ya Mbinga amepita kwenye barabara ya kiwango cha lami iliojegwa na nchi ya China kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania.
 
 Ziara hiyo ya balozi wa China kutembelea mkoa wa Ruvuma umekuwa ni mwaliko rasmi wa mbunge wa jimbo la Peramiho kwa tiketi ya chama cha mapinduzi  Jenista Mhagama ambaye aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutumia fursa hiyo ya ujio wa balozi huyo kwa kufanya kazi zaidi katika kilimo kwa sababu balozi huyo ameahidi kulifanya zao la mahindi kuwa zao la kibiashara.
 
 Alisema kuwa kilimo cha kisasa ndicho kinachoweza kuwakwamua zaidi kuichumi na kuondokana na wimbi la umasikini linalowakabili pia aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo na misaada iliyotolewa kwao na balozi huyo kama changamoto kwao katika kujikwamua kiuchumi na kupambana na umasikini uliopo.