Sunday, April 21, 2013

POLISI YAMSAKA MFANYA BIASHARA WA MADINI ANAYEDAIWA KUMPIGA RISASI POLISI

1
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara,Akili Mpwapwa

NA Gladness mushi,Manyara

JESHI la polisi Mkoani Manyara linamtafuta mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara Lawi Abayo (33) anayedaiwa kumpiga risasi ya kichwa askari polisi na kumuua.

Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara,Akili Mpwapwa alisema Abayo anadaiwa kumpiga risasi ya kichwa askari wa kituo cha polisi Mirerani PC Joseph Tairo G.7037 wakati akimpeleka mhalifu kituoni.

Alisema askari huyo alifariki juzi baada ya kupigwa risasi Aprili 7 mwaka huu wakati alipomkamata mhalifu aliyekuwa anafanya vurugu kwenye baa ya Kazamoyo Reasort (Kwa mdava) na kuanza kumpeleka kituo cha polisi Mirerani.

Alisema baada ya kutembea naye kama mita 20 kutoka kwenye baa hiyo ndipo Lawi akiwa na gari jeusi aina ya Prado akashuka ghafla na kumpiga risasi ya kichwani askari wetu na kisha akamchukua huyo mhalifu na kuondoka naye.

“Baada ya kupigwa risasi kwa askari huyo aliyekuwa na mwenzake PC Martin G G.8523,alipelekwa kwenye kituo cha afya Mirerani kisha hospitali ya rufaa ya KCMC mjini Moshi na kuhamishiwa Muhimbili alipofia,” alisema Mpwapwa.

Alisema wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo anayedaiwa kumpiga risasi askari huyo na hadi hivi sasa wanashikilia gari aina ya Prado lenye namba T671 ATK  lililotumika kufanya tukio hilo na kumkimbiza Abayo.

Alitoa wito kwa wote watakaomuona Abayo watoe taarifa kwa polisi kwani inadaiwa alikimbilia kati ya jijini Dar es salaam,Musoma na Rorya mkoani Mara au Kisumu na Nairobi nchini Kenya.