Tuesday, April 9, 2013

WATAKIWA KUWEKEZA KATIKA VYUO VYA UFUNDI

 
MKUU WA WILAYA YA MBOZI DR.MICHAEL KADEGHE

SERIKALI imewataka wamiliki  wa shule na vyuo binafsi  kuwekeza katika ujenzi wa vyuo vya  elimu ya  mafunzo ya ufundi, ili kukidhi hitaji kubwa la vijana wanaomaliza elimu ya sekondari ambao wangependa kujiendeleza ili wajiajiri.

Rai hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,  Dk. Michael Kadeghe  katika Mkutano Mkuu  wa taifa wa mwaka wa  Wakuu na Wamiliki na Mameneja wa Shule za Msingi, Sekondari na vyuo nchini  (TAMONGSCO).

Dk. Kadegde alisema serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika sekta ya elimu, lakini ni vema jumuiya hiyo ikawekeza katika ujenzi wa vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi ili kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.

Akizungumzia ada kubwa zinazotozwa na shule binafsi, Dk. Kadeghe alisema serikali inatambua wametumia gharama kubwa katika ujenzi na  uendeshaji, lakini ni vema  Tamongsco wakazishauri bodi za shule na vyuo husika kufanya  tafiti na kujua hali halisi ya kipato cha mzazi ama mlezi wa mwanafunzi, ili ziweze kutoa uamuzi jinsi ya kuwasadia wanafunzi wasikatishwe masomo kwa kukosa ada.

‘Tamongsco ifanye utafiti wa kina kuelewa gharama halisi ya kumsomesha mwanafunzi kwa mwaka, ili mfikie makubaliano ya pamoja juu ya kiwango ambacho kinafaa kutozwa katika shule zisizo za serikali bila kumuumiza mzazi,” alisema  Dk. Kadeghe.
Mwenyekiti wa Tamongsco Taifa Mahmoud K.  Mringo, alisema moja ya sababu ya kutoza ada kubwa ni kutokana na gharama kubwa za uendeshaji ikiwemo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).