Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi , akimkabidhi cheti cha
usajili wa utaalamu wa afya ya mazingira , Mary Swai , ambaye ni
Mwenyekiti mpya wa awamu ya pili ya Baraza la Usajili wa
Wataalam wa Afya ya Mazingira nchini, (jana) wakati wa uzinduzi wa
baraza hilo , uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi , akizungumza na
wajumbe wa Baraza la Usajili wa Wataalam wa Afya ya Mazingira
nchini, (jana) wakati wa uzinduzi wa baraza hilo , uliofanyika jana
jijini Dar es Salaam.
………………………………………………..
Frank John na Hassan Silayo- Maelezo
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein
Mwinyi amewataka wajumbe wa Baraza la Usajili wa Wataalam wa Afya ya
Mazingira nchini, kufanya kazi kwa kujituma na ushirikiano ili
kupambana na changamoto zinazokabili sekta hiyo na kuzuia maambukizi
ya magonjwa.
Dk. mwinyi aliyasema hayo(jana)
wakati wa uzinduzi wa baraza hilo uliofanyika jana jijini Dar es salaam
ambapo alisema sekta ya afya na ustawi wa jamii inakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo ongezeko la milipuko ya magonjwa kutokana na
uchafuzi wa mazingira.
Alibainisha kuwa afya ya mazingira ni suala
mtabuka ambalo linahitaji ushirikishwaji wa wadau wa sekta ya afya ya
mazingira ili kutoa matokeo yenye tija na ubora wa hali ya juu katika
kupambana na magonjwa hayo.
Aliongeza kuwa serikali inatarajia kwamba
kwa kutumia baraza hilo huduma ya afya ya jamii itatolewa kwa wananchi
kwa viwango vinavyotakiwa na hivyo, kuboresha maisha ya wananchi kwa
kusimamia na kudhibiti utoaji wa huduma ya afya ya mazingira kwa misingi
ya haki.
“Pia wataalam wa kada hii watajiendeleza na
kufikia kiwango cha juu cha elimu tofauti na miaka iliyopita ampapo
wengi waliridhika na kubaki katika eneo moja kwa muda mrefu na
kusababisha kudumaa kwa taaluma,alisema Dk.Mwinyi.
Alisema kwa kufanya , hivyo upo uwezekano
mkubwa wa kupunguza ongezeko la kasi ya magonjwa, vifo na madhara
mengine katika jamii yatapungua ikiwa huduma ya afya ya jamii
itaboreshwa.
Naye Mwenyekiti wa baraza hilo , lililomaliza
muda wake Bwana Fabian Magoma alisema linakabiliwa na changamoto za
upungufu wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za baraza na
ukosefu wa mitaala hivyo linahitaji ushirikiano wa karibu na taasisi
zinazoandaa mitaala ya elimu nchini.
Magoma alishauri baraza hilo, liangalie
sheria zinazohusiana na afya ya mazingira, ili waweze kutambua taaluma
hiyo. Huku akiongeza kuwa watu wanaoteuliwa kufanya kazi hiyo wawe ni
wa kada hiyo.
Kwa upande wake mjumbe wa baraza jipya Haji
Mdemu alishauri serikali kuzingatia mbinu za zamani za afya mazingira ,
kuzifufua ili kuimarisha afya mazingira na uwajibikaji wa maafisa afya.
Baraza hilo lilizinduliwa rasmi mwaka 2009
ikiwa ni matokeo ya sheria ya kusajili wataalam wa afya mazingira ya
mwaka 2007 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
likiwa na majukumu ya kusajili, kudhibiti nidhamu kiutendaji katika kada
ya afya ya mazingira pamoja na kumshauri waziri husika juu ya masuala
yote yahusuyo afya ya mazingira nchini.