Tuesday, April 9, 2013

Wananchi Loliondo waapa kumwaga damu wakitetea ardhi yao

 

WANANCHI wa Wilaya Loliondo, mkoani Arusha, wamesema wapo tayari kumwaga damu wakitetea haki ya ardhi yao waliyoirithi kutoka kwa babu zao, endapo Serikali itaendelea na mpango wa kuigawa kwa wawekezaji.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao Jijini Dar es Salaam jana, Diwani wa Kata ya Ololosokwan, Yanick Ndoinyo, alisema hawatakifumbia macho kitendo cha kupokonywa ardhi yao, badala yake wataingia msituni kupambana ili kuhakikisha haki inatendeka.

Alisema wana umiliki halali wa ardhi waliyopewa kupitia sheria ya ardhi namba 3 ya mwaka 1923 na sheria ya ardhi ya mwaka 1999 na Katiba ya Nchi ambayo ilisajili vijiji vyote, ikiwemo tarafa ya Loliondo.

“Tumeshangazwa na kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, aliyoitoa Machi 21 mwaka huu, kwa umma na kudai kuwa Serikali imeamua kupunguza ukubwa wa eneo hilo ili kutatua migogoro iliyopo, kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti , Ngorongoro na Pori Tengefu, jambo ambalo si kweli na ni upotoshaji wa taarifa kwa umma,” alisema.

Alieleza kuwa mgogoro wa eneo hilo umedumu kwa muda mrefu tangu mwaka 1992, wakati Serikali ilipoingia mkataba na kampuni ya Otterlo Business Corporation (OBC), ya kutumia ardhi ya kijiji bila ridhaa ya wanakijiji husika.

Alisema mgogoro huo ulisababisha makazi ya wananchi na mali zao kuchomwa kwa lengo la kulazimisha kumpisha mwekezaji huyo apate fursa ya kuishi katika ardhi ya kijiji bila ridhaa yao.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Soitsambu , Daniel Ngoitiko, alisema Waziri Kagasheki amepotosha umma kwamba eneo hilo ni la muhimu kwa sababu ya uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti, yaani vyanzo vya maji, mazalia ya wanyama na mapito ya wanyama.

“Hapa jamani waziri anatugawia ardhi au anatupokonya, jambo hili ni vyema likawa la wazi na likaangaliwa kwa undani zaidi,” alisema diwani huyo.

Aidha ameiomba Serikali kuacha kuzungumzia masuala hayo ya wilaya hiyo, kwani ni ya upotoshaji na kuacha vitisho kwa wananchi na waandishi wa habari wanaofuatilia mgogoro huo.


chanzo http://mtanzania.co.tz