Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, Nadhiru Kinyama akizungumza na mwandishi wa Thehabari.com
Mwanafunzi Mwenjuma Magalu (16), mstari wa pili kulia wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo
Na
Thehabari.com, Handeni
MWANAFUNZI
wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, Mwenjuma Magalu (16) amejikuta akibeba mzigo wa kulea familia baada ya familia
hiyo kutelekezwa na babayake.
Mwanafunzi
huyo anayeishi katika Kijini cha Msasa amejikuta katika hali hiyo ngumu baada
ya mama yake mzazi, Hadija Magalu kufariki dunia ambaye ndiye aliyekuwa akiihudumia familia hiyo baada ya mzazi
mwenzake (mumewe) kuitelekeza miaka minne iliyopita.
Mama huyo (Hadija
Magalu) alifariki dunia Agosti, 2013 kwa matatizo ya uzazi na kuiacha familia
hiyo ya watoto watatu aliyokuwa akiihudumia chini ya ulezi wa mamayake mzazi, Bibi
Amina Mohamed.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni kijijini Msasa, mwanafunzi Magalu
alisema amelazimika kuilea familia hiyo baada ya bibi yake aliyeachiwa familia
hiyo kuugua ugonjwa wa TB na kushindwa kuendesha shughuli za kilimo na
nyinginezo kuisaidia familia hiyo.
“Bibi ndiye
aliyekuwa akitupikia, tutafutia chakula na tulikuwa tukishirikiana naye hata
kulima…lakini kazi hizo zote kutokana na afya yake hawezi kuzifanya,
ninalazimika kuzifanya mwenyewe. Japokuwa nipo shuleni lakini natakiwa kujua
tutakula nini tunapata wapi pesa ya chakula na shughuli nyingine za familia,”
alisema Magalu akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Alisema
familia yao hutegemea kilimo lakini wakati mwingine hulazimika kwenda kutafuta
vibarua vya kufanya ili kupata pesa ya kula yeye pamoja na bibi yake. Aidha
aliongeza kuwa wadogo zake wawili ambao awali alikuwa akikaa nao amelazimika
kuwapeleka kwa mjomba wake baada ya kuona hali ni ngumu. Hata hivyo alisema
wajomba zake nao hali yao ni ngumu hivyo wanashindwa kuhudumia familia hiyo.
Akizungumzia
hali ya maisha ya familia hiyo Bibi. Amina Mohamed ambaye kwa sasa ni mgonjwa
wa TB alikiri mwanafunzi huyo kuwa na majukumu mazito ya familia ambayo awali
alikuwa ameyabeba yeye baada ya mwanaye kufariki dunia.
“Kweli mtoto
huyu anaelemewa na malezi ya familia hii lakini sina cha kufanya kwa kuwa mimi
ni mgonjwa wa TB na nimeshauriwa nisifanye kazi kwa sasa, hivyo kuanzia kupika,
kulima shambani na hata kutafuta cha kula anafanya yeye baada ya kurudi
shuleni,” alisema bibi huyo.
Mwanafunzi
huyo ambaye anasomeshwa na msamaria mmoja aliyejitokeza baada ya familia yao
kushindwa kumlipia ada amewaomba watu walioguswa na maisha ya familia hiyo
kumsaidia.
Akizungumza
hivi karibuni Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, Nadhiru
Kinyama alikiri hali ngumu kwa kijana huyo kutokana na mazingira ya familia yao
na kuongeza anahitaji kusaidiwa hata fedha za kujikimu na gharama zingine za
masomo.