Thursday, April 11, 2013

MHIFADHI KIONGOZI MAKUMBUSHO YA TAIFA MAJIMAJI SONGEA AWATAKA WATANZANIA KUJITOKEZA KUTEMBELEA MAKUMBUSHO YA MAJI MAJI

Toka kulia ni Bw. Balthazali Nyamusya  Mhifadhi Kiongozi Makumbuaho ya Taifa Maji Maji Songea akitoa historia ya vita ya Maji Maji kwa mmoja wa wageni waliotembela hapo ambaye ni Bw.Likati thomas pia ni graphic designer wa daraja
 Sehemu hii ndipo walipokuwa wananyongewa mashujaa wa vita vya Maji Maji, mmoja mmoja alikuwa anapandishwa kwenye kitanzi kisha kunyongwa, Awali hapa palikuwepo na mti ambao ulitumiwa lakini kutoka na mti huo kuzeeka ulianguka na leo hii umejengwa mnala kama kielelezo husika.
Mmiliki wa demashonews akiwa katika jumba lenye vifaa mbalimbali vya historia ya Maji Maji ambavyo mashujaa  walitumia kupigania, Viafaa hivi vipo vimehifadhiwa katika jumba la makumbusho.
......................................................................
Kupitia Sherehe za kila mwaka za Kumbukumbu ya Mashujaa zenye kauli mbiu ya Mkoa (Mji wa Kihistoria na Kishujaa) ambazo zilibadilika na kuwa tamasha la utalii wa Kitamaduni la Kitaifa la siku tatu yaani tarehe 25-27 Februari ya kila mwaka. 

Wakazi wa Mkoa wa Ruvuma wameanza kuhamasika kutembelea Makumbusho haya baada ya kujifunza kutokana na matamasha yanayofanyika kila ifikapo Februari 25-27. Wamebadilisha fikra zao na kuona kuwa Makumbusho si mahala tu pa kuhifadhi vitu vya kale na visivyo na maana bali . “ Makumbusho”  kama kituo cha elimu.  Mtu atembeleapo Makumbusho anaona mambo mengi ambayo  anaweza kujifunza.  

Bw. Balthazali Nyamusya ambaye ni Mhifadhi Kiongozi Makumbuaho ya Taifa Maji Maji Songea akizungumza na mwandishi wa demashonews amesema kuwa makumbusho  haya ni kituo cha elimu kwani wageni mbalimbali toka  ndani ya nchi na nje ya nchi hufika mahala hapa kujifunza juu ya historia ya vita vya majimaji.
 Pia wanafunzi hutembelea Makumbusho kama ziada ya elimu ya kiada wapatayo mashuleni, wale wa sekondari na vyuo hutembelea Makumbusho na kufanya kazi miradi na tafiti.

"Nachukua fursa hii kuwaalika wageni toka mataifa mbalimbali wakiwemo wananchi wote na wenyeji wa   Mkoa wa Ruvuma wazidi kutembela Makumbusho haya , hivyo kuenzi urithi wa utamaduni wetu hususani kumbukumbu za vita hivi vya Kihistoria kusini mwa Jangwa la Sahara, vita iliyohusisha jamii nyingi ambazo kwa nguvu moja na moyo wa uzalendo walipambana kupinga utawala wa mkoloni wa Kijerumani". 

Makumbusho haya ya Maji yalianzishwa na kufunguliwa Rasmi tarehe 06 Julai 1980. Lengo kuu  la kuanzisha Makumbusho haya ni kutunza kumbukumbu ya historia ya vita vya Maji Maji vya (Julai 1905-Agosti 1907) yalijengwa mahali ambapo Mashujaa wetu wa Vita  vya Maji Maji hususani kutoka Mkoa wa Ruvuma Walizikwa.
Katika eneo hili la mashujaa maarufu kama (Hero- square) kuna makaburi mawili ya Mashujaa wetu; Moja ni lile la Halaiki ambamo zaidi ya watu 60 walizikwa baada ya kunyongwa. Mashujaa hawa walionyongwa siku ya 27/2/1906 na pia kaburi jingine lilopo pembeni yake ni la Nduna (Sub-Chiesf) Maarufu Songea Mbano ambaye hata mji wa Songea ulibatizwa kwa jina lake.

Sehemu hii ni muhimu sana katika historia ya nchi yetu na Dunia kwa ujumla kwani imebeba historia ambayo inatukumbusha chimbuko la Mwafrika-Mtanzania kutambua na kupinga ukoloni na kutawaliwa, kiasi ambacho kilipelekea kuwagharimu Maisha yao katika Vita vya Maji Maji. Kwa takwimu ambazo zipo mpaka leo inaonyesha zaidi ya ya Watanzania 75,000 walipoteza maisha katika ukanda wa kusini-Mashariki maeneo ambayo vita vilipiganwa na 1,000 miongoni mwao wakitokea katika Mkoa wa Ruvuma. 


Hapana  shaka kwamba vita vya Maji Maji ni kumbukumbu muhimu katika historia ya Tanganyika inayostahili kuheshimiwa na yeyote anayethamini utu, haki, heshima na usawa . Vita vya Maji Maji ni kielelezo halisi cha Watanzania kukataa utawala wa kikoloni.
 

Karibu Ruvuma karibu Tanzania.
.....................................................
...........................
.................
............