Monday, April 22, 2013

Watu sita wanusurika kifo ajali ya gari Songea

Na Nathan Mtega,Songea
 
 WATU sita wamenusurika kifo baada ya gari waliokuwa wakisafiria kutoka Songea kuelekea jijini Mbeya kupinduka katika eneo la Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma na kusababisha watu hao kujeruhiwa na kukimbizwa katika kituo cha afya cha Madaba kilichopo wilayani Songea.
 
 Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo walimuambia mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu kuwa ajali hiyo ilitokea Aprili 21 mwaka huu majira ya saa 3 asubuhi ambapo gari aina ya NOAH yenye namba za usajili T 627 BUX iliyokuwa ikiendeshwa na dereva Joel Mwakopisya(57)  mkazi wa Mbeya lilipinduka katika eneo hilo na kusababisha majeraha kwa watu sita .
 
Aidha taarifa kutoka katika kituo cha  afya cha Madaba wilayani Songea imewataja majeruhi waliofikishwa katika kituo hicho kuwa ni Erika Kihwanja(79) ambaye alikuwa anatolewa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma kupelekwa jijini Mbeya ambae alizimia baada ya tukio hilo na wengine ni Obadia Mwaikosya(55),Grace Daud(29), Luth Joseph(19) na Joshua Said(10) mwanafunzi wa darasa la tatu latika shule ya msingi De Paul ya mjini Songea.
 
 Aidha majeruhi watano wameletwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma ambapo kwa mujibu wa Kaimu mganga mkuu mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt Mahtew Chanangula aliwataja Grace Daud na Erika Kihwanja kuwa ndiyo wenye halimbaya na Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Deisdedit Nsimeki amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuhahidi kutoa taarifa zaidi baada ya uchunguzi kufanyika.