Thursday, April 4, 2013

Watu 45 kushtakiwa vurugu za nani achinje huko Tunduma

 

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani

Mbeya na Dar es Salaam. Watu 45 watafikishwa mahakamani wakihusishwa na vurugu zilizozuka juzi katika Mji wa Tunduma.

Vurugu kubwa ziliibuka juzi kwenye Mji mdogo wa Tunduma ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya kwa baadhi ya wakazi kuwa na mvutano mkali kuhusu nani anayepaswa kuchinja mifugo baina ya waumini wa Kikristo na Waislamu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alisema jana watu 94 ndiyo waliokamatwa kutokana na vurugu hizo.

Diwani alisema watu 49 wameachiwa kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea wakati waliobakia 45 ndiyo watafikishwa mahakamani. Vurugu hizo za Tunduma zilihusisha uchomaji wa matairi barabarani, kuweka mawe na magogo kwa lengo la kufunga barabara na kusababisha shughuli za kiuchumi kusimama na wananchi kujifungia ndani kwenye nyumba zao.

Diwani alidokeza, hata hivyo, hali ya utulivu imerejea kama kawaida na kwamba tayari wananchi wanaendelea na shughuli zao za kawaida ikiwa ni pamoja na eneo la mpakani.

“Kwa sasa hali imerudi kama kawaida na tumetangaziwa kuwa tuendelee na shughuli zetu na kwamba hali itakapobadilika tutoe taarifa polisi...Wametutaka kila mmoja kuwa na ulinzi hivyo watu wameshaanza kujitokeza barabarani na kufungua biashara zao,” alisema mkazi wa Tunduma aliyejitambulisha kwa jina la John Mwasyeba.

Mbatia alonga
Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepanga kukutana na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kiislamu na Kikristo nchini ili kumaliza tofauti zilizopo zinazojitokeza kati ya waumini hao.

Katika mkutano wao jana, TCD ambayo ni muungano wa vyama vya siasa vyenye wabunge bungeni vikiwemo CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi, TLP, UDP na CUF vile ambavyo havina wabunge pia vina mwakilishi mmoja katika kituo hicho.
Kituo hicho kimesema kuwa kimechukua uamuzi huo baada ya nchi kukumbwa na migogoro ya kidini.

Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia alisema jambo hili likiachwa litaligawa taifa na kwamba migogoro hiyo haina tija kwa taifa: “Amani ikitoweka katika taifa letu watakaoathirika ni Watanzania wote, ni lazima tukutane na viongozi hawa ili kujua tatizo ni nini, kufungua ukurasa mpya.”

Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alisema watakutana na viongozi hao Aprili 23 na 24 mwaka huu, tayari walishaelezwa jambo hilo na wamekubali.

Kwa nyakati tofauti, viongozi mbalimbali wa dini nchini wamekuwa wakiitaka Serikali kukaa meza moja na viongozi hao, baadhi ya viongozi waliotoa kauli hiyo ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo pamoja na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadji Mussa Salum.

Vurugu hizo za Tunduma zimejitokeza ikiwa ni siku tatu tu tangu Rais Jakaya Kikwete aonye kuwa vurugu zenye sura ya udini ni hatari na zinaweza kuvuruga amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi nchini.