Songea Mbano
Na Stephano Mango, Songea.
HUWEZI kuilezea na kuikamilisha historia ya
vita ya Majimaji na ukombozi wa nchi yetu bila kumtaja shujaa wa kabila
la wangoni Nduna Songea Mbano ambaye jina lake lilipewa hadhi ya kuuita mji wa Songea kutoka kwenye jina la Ndonde mwaka 1906.
Kiongozi huyo alikuwa ni miongoni mwa
wasaidizi ( Nduna) 12 wa Chifu wa kabila la wangoni (Nkosi) chifu Mputa
bin Gwezerapasi Gama.
Ambapo wasaidizi wake wengine walikuwa ni
Mgendera Mawaso Gama, Kohongo Magagura, Mputa Mkuzo Gama, Magodi Mbamba
Mbano, Mtekateka Muyamuya Tawete, Fratela Fusi Gama.
Manduna wengiwe ni Maji ya kuhanga Komba,
Zimanimoto Gama, Mpambalyoto Soko Msalawani, Mtepa Hawaya Gama na Nduna
Mkomanile ambaye alikuwa ni mwanamke pekee kuwa nduna.
Nduna Songea Mbano alikuwa ni maarufu kuliko manduna wenzake na hata chifu Mputa Gama alikuwa anamtegemea sana katika kuwaongoza Manduna wenzake na wapiganaji wa vita ya Majimaji kiujumla.
Mhifadhi kiongozi wa Makumbusho ya Taifa
Maji maji Songea Philipo Maligissu akizungumzia maisha ya Nduna Songea
Mbano katika viwanja vya Makumbusho hayo,alisema kuwa Songea Mbano akiwa
miongoni mwa manduna alitokea kuwa maarufu sana ukilinganisha na
wenzake 11 ambapo sifa kubwa iliyo mpa umaarufu ili kuwa ni ueledi na
ushadi wake wa kuandaa mikakati ya kivita, na maamuzi mazito
yasiyoteteleka na kuyasimamia maamuzi hayo kikamilifu.
Kwa umakini mkubwa Nduna Songea Mbano
aliweza kufanya kile alichokuwa akikiamini na uthibitisho wa jambo hilo
ulianza kujitokeza julai 12, mwaka 1897 katika viwanja vya Bomani kwa
mkuu wa Wilaya wa wajerumani luteni Engelhardt.
Maligissu anasema kuwa kwa rekodi zilizopo
zinaonyesha kuwa tarehe hiyo Nduna Songea Mbano alionekana kuwa ni mtu
wa kipekee katika idadi ya Manduna 11 ambao walikuwa wasaidizi wa chifu
Mputa Gama kwa kitendo chake cha kubisha wazi wazi tamko la utawala mpya
wa wajerumani la kutaka wangoni wakomeshe biashara ya utumwa.
Siku hiyo ilikuwa ni siku rasmi ambayo
utawala wa kikoloni ulikuwa unaanzishwa katika mji wa Songea wakati huo
ulikuwa unaitwa Ndonde na Mkoa wa Ruvuma kiujumla chini ya Luteni Engelhardt wa Jeshi la Kijerumani ambaye alikuwa ndiye Mkuu wa Jeshi kwa kanda ya Kusini.
Wajerumani walipofika kuanzisha makoloni yao katika maeneo ya ukanda wa kusini walikutana na msuguano mkubwa kutoka kwenye tawala za kiafrika hususani tawala za wangoni.
Maligissu anasema kuwa wangoni walikuwa na
tabia ya kwenda mikoa ya Lindi na Mtwara kuvamia na kuchukua mateka na
kuwaleta Songea kuwafanyisha shughuli mbalimbali katika maeneo yao ya utawala.
Tabia hiyo ya wangoni iliwachukiza sana wajerumani kwani wajerumani walikuwa wanaheshimu sana makubaliano yaliyofikiwa kutoka kwenye mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 hadi 1885.
Katika mkutano huo moja ya makubaliano
yaliyofikiwa ni pamoja na kila nchi yenye koloni barani Afrika ni lazima
ikomeshe biashara ya utumwa na kwa kuwa wajerumani walikuwa
wamejiimarisha sana katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Hivyo walipokuja Ruvuma
wakatoa tamko kwa wangoni kuwa hairuhusiwi na haitaruhusiwa tena kwenda
Lindi,Mtwara na maeneo mengine kuchukua mateka na kwamba mateka wote
waliochukuliwa na wangoni waachiwe huru.
Baada ya wajerumani kutoa tamko hilo ndipo Nduna Songea Mbano alipojitokeza waziwazi na kusimama kujibu hoja iliyotolewa na wajerumani kuhusiana na tamko hilo.
Nduna Songea Mbano alisema kuwa utawala wa kabila la wangoni hauwezi kutekeleza tamko hilo na kwamba msimamo wao ni kutoutambua utawala mpya wa kijerumani na tamko lao.
Aliendelea kusema kuwa ujio wa utawala wa
wajerumani na kutoa tamko hilo kwa wangoni una lengo la kudhoofisha
utawala wa Machifu na Manduna katika maeneo yao kwa kufuata kanuni zao
za kimila na kitamaduni.
Kuanzia hapo wajerumani walimuona Nduna Songea Mbano kuwa ni mtu hatari sana katika utawala wao mpya na walimuweka alama maalumu na kuanza kumfuatilia nyendo zake.
Kwa sababu alionekana kuwa kiongozi shupavu na mwenye misimamo mikali na anayezingatia heshima na utu wa kabila lake bila kuyumbishwa.
Alionekana kuwa ni mtu wa pekee mwenye
uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira yoyote kwa kushirikiana na
wananchi wake ambao walikuwa wana mheshimu sana na kumsikiliza.
Maligissu anaeleza kuwa Nduna Songea Mbano
alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha wananchi wake na kuwa na umoja,
upendo na mshikamano na kwamba alikuwa akiwaelekeza jambo wanalifanya
kwa umakini na kwa ukamilifu.
Anaendelea kusema kuwa kuanzia hapo Nduna
Songea Mbano aliendelea kujizolea umaarufu mkubwa na wajerumani baada ya
kuona hivyo na kitendo cha nduna Songea kutamka kuwa yupo tayari kwa
lolote lile na hawezi kukubali kuona tawala za kiafrka zinadharauliwa na
wakoloni kwa namna yeyote ile.
Waliamua kuwaalika Machifu na Manduna wote
Julai 13 mwaka 1897 Bomani kwa mkuu wa Wilaya wa kwanza katika nchi ya
ungoni ambaye pia mkuu wa jeshi la wajerumani katika nchi ya ungoni
Luteni Engelhardt na kuwaambia kuwa mtu yoyote katika eneo lake atakaye
kaidi amri yeyote kutoka kwa uongozi mpya wa wajerumani basi atapigwa
risasi, kunyongwa hadi kufa au kufungwa maisha .
Siku hiyohiyo Machifu na Manduna
walichukuliwa hadi juu ya mlima wa shabaha wa chandamari uliopo katikati
ya mji wa Songea na kuwaonyesha nguvu ya risasi inavyoweza kufanya kazi
katika mwili wa binadamu na kwamba silaha za kijadi na kimila za
wangoni haziwezi kufua dafu mbele ya silaha hizo.
Licha ya wajerumani kutoa mkwara na
vitisho vingi Nduna Songea Mbano aliendelea kushikilia msimamo wake wa
awali wa kuchukia utawala wa wajerumani na kuutetea utawala wa kiafrika
mpaka vilipo kuja kutokea vita vya Majimaji.
Nduna Songea Mbano alitoa ushindani mkubwa sana
katika vita hivyo na alionyesha ustadi mkubwa kwenye mapigano na katika
sehemu zote ambazo wajerumani walipigana wameandika kuwa hawakupata
ushindi mkubwa kama waliopata katika Mkoa wa Ruvuma zamani nchi ya ungoni.
Ambapo viongozi wao hawa kuwa wanafiki
kwani walijitoa kikwe likweli kusaka ukombozi wa kweli na hadhi ya
tamaduni zao mpaka dakika ya mwisho, ndio maana idadi ya watu
walionyongwa katika historia ya nchi yetu walitoka katika himaya ya
Nduna Songea Mbano na ushahidi upo wazi kuwa watu 67 walihukumiwa
kunyongwa hadi kufa akiwemo Nduna Songea Mbano.
Katika kuonyesha kuwa Nduna Songea Mbano
alikuwa na uwezo wa kufanya mambo kwa uweledi mkubwa bila kusaliti
dhamira yake kuanzia mwaka 1897 alianza kuandaa jeshi lake la kupambana
na utawala wa wajerumani.
Akaanza kuchukua watu wake na kuwapeleka
juu ya mlima wa chandamari, kufanya nao mkutano na kutoa mafunzo ya
kivita na kuwaelekeza kwa nini wanawachukia wajerumani.
Katika mlima huo ndipo alipoeleza kwa kina
madhara ya kuukubali utawala wa wajerumani na kutoa ahadi kwa wananchi
wake ya kuwaondoa wajerumani kwa lazima na kwamba alisema kuwa eneo hilo
ni lao na wamekuwa wakiishi siku zote chini ya utawala wao sasa
inakuwaje waletewe utawala mpya wakati hawahuitaji.
Chokochoko hizo zilizaa vita vya Majimaji
na wakati mapigano yakiendelea wajerumani walianza kumtafuta Nduna
Songea Mbano ili wamkamate na kufanya nae mazungumzo ya maridhiano.
Kumbe Songea Mbano alikuwa amejificha
kwenye pango kubwa lililopo kwenye mlima wa chandamari na usiku hukutana
na askari wake nje ya pango hilo na kuwapa mafunzo zaidi ya kivita.
Maligissu anaeleza kuwa Nduna Songea Mbano
alikuwa anaishi na Ndugu zake katika eneo la Mateka lililopo katika eneo
la Manispaa ya Songea na wakati wa vita ndipo Songea Mbano alikuwa
anajifisha katika pango hilo ili wasimkamate mpaka atakapotimiza malengo yake.
Wajerumani walipoona wanaendelea kupata
madhara makubwa kutokana na vita hivyo waliamua kuwakamata ndugu na
familia yake, chifu Mputa Gama na Manduna wengine na kuwafunga gerezani
kwa lengo la kumdhoofisha Nduna Songea Mbano.
Baada ya wajerumani kumdhoofisha Nduna Songea Mbano alipata taarifa zote na akaamua kutoka kwenye pango hilo na kwenda kwa wajerumani na kutaka watu wake waachiwe ili mapigano yaendelee.
Ndipo naye alipokamatwa na kuwekwa gerezani
na kwamba utawala wa wajerumani waliamua kuwa hukumu wafugwa hao
kunyogwa hadi kufa akiwemo chifu wa kabila la Wangoni.
Wafungwa hao waliamuliwa kuchimba shimo kubwa bila kujua kuwa shimo hilo
ndilo litakalotumika kuwa kaburi lao na ilipofika siku ya kunyongwa
walinyongwa kwa zamu siku mbili na maiti zao kwenda kuwekwa kwenye
kaburi hilo hadi walipofikia 66 ndipo walizikwa kwa pamoja kwenye kaburi hilo.
Nduna Songea Mbano walimuacha ili aweze kuwasaidia kufikisha malengo yao kwa wananchi kwani waliamini kuwa yeye ni kiongozi jasiri na anayependwa na watu wake na kusikilizwa vizuri.
Toka siku hiyo walipomuacha bila kumnyonga Nduna Songea Mbano aliwasumbua sana wajerumani na kutaka naye anyongwe kama ndugu zake kwani haoni sababu ya yeye kuishi wakati ndugu zake wamekufa na kusema kama hawataki kumnyonga basi hataki kula wala kunywa chochote mpaka afe.
Ndipo wajerumani walipoamua kumnyonga na
kumzika katika kaburi la pekee yake wakiamini kuwa ni mtu wa pekee
mwenye ushujaa na maamuzi mazito na misimamo isiyoyumba na walimuenzi
kwa kubadilisha jina la mji wa Ndonde na kuubatiza jina la Songea ambapo
mpaka sasa linatumika kuuita mji huo wenye hazina kubwa ya historia na
utalii wa kitamaduni
Kila mmoja wetu hana budi kujiuliza ni
mafundisho yepi anaweza kuyapata katika historia ya nchi yetu na mchango
mkubwa alioutoa Nduna Songea Mbano na je kizazi kilichopo tunao ule
moyo wa ushujaa , uzalendo heshima na usawa kama ilivyo kuwa kwa mababu
zetu basi inatupasa tutimize wajibu wetu kikamilifu ili vizazi vijavyo
viweze kunufaika na uwepo wetu duniani.