Sunday, April 7, 2013

BABA 'ANYONGA' WANAWE WATATU HUKU MAMA AKISHUHUDIA KATAVI..

Kamanda Dhahiri Kidavashari.
Ukatili wa kusikitisha! Watoto watatu wa familia moja, wameuawa kikatili kwa kunyongwa huku mama yao akishuhudia, na miili yao pamoja na mama yao akiwa hai, wakatumbukizwa katika kisima cha maji.

Kabla ya mauaji hayo, baba wa watoto hao, Justine Albert (24),  anayetuhumiwa kufanya unyama huo, inadaiwa alimfunga kamba mkewe na kumziba mdomo kwa kitambaa ili asipige kelele, kisha akaanza kuwanyonga watoto wake wote watatu kwa zamu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, alisema   mauaji  hayo  ya kikatili yalifanyika juzi saa 11:30 alfajiri, katika Kijiji cha Majimoto, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Mlele mkoani humo.

Kisa cha kufanya mauaji hayo kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, ni mzozo wa mtuhumiwa na mkewe, Jacqueline Luvika (21), kwamba baadhi ya watoto hao mama huyo kazaa na jirani yao.
Watoto hao ni Frank Justine (6), Elizabeth Justine (4) na kitinda mimba Maria Justine, mwenye umri wa miezi minne.

Baada ya kuwanyonga watoto hao, inadaiwa baba huyo alibeba miili ya watoto Frank na Eliza, na kwenda kuwatumbukiza kwenye kisima cha jirani yao, Kawaida Jonas.
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Kidavashari, mtuhumiwa baada ya kuwatumbukiza watoto hao kisimani, alimfungua kamba mkewe na kumtoa kitamba  alichomziba mdomoni, kasha akamburuta hadi kwenye kisima hicho  na kumtumbukiza.

Baada ya matukio hayo yanayiodaiwa kufanyika alfajiri, kulipopambazuka baadhi ya wakazi  wa kijiji  hicho waliodamka kwenda katika shuhuli zao, waliuona mwili wa mtoto ukiwa umetelekeza kando ya njia na kutambua kuwa ni Maria ambaye  ni  kitindamimba  katika familia hiyo. 

Inadaiwa wakazi hao walisitisha safari yao na kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa kumpatia  taarifa hiyo ya kuhuzunisha, huku wakiuliza mama  wa mtoto  aliko.
Kamanda Kidavashari alidai mtuhumiwa aliwaeleza wakazi hao kuwa mama wa mtoto huyo, alikuwa ametoroka kwenda kusikofahamika na watoto wote.
Majibu hayo ‘rahisi’ kwa mujibu Kamanda  Kidavashari, yalisababisha  wakazi hao wamtilie shaka mtuhumiwa, wakaamua kutoa  taarifa kituo cha Polisi kijijini hapo  ambao  walifika  ulipo mwili wa  mtoto Maria. 

Wakati wakiwa katika eneo la tukio, Kamanda  Kidavashari alidai walibaini alama za mburuzo ardhini, wakaanza kuifuatilia ikawafikisha kisimani na wapofungua mfuniko wa  kisima hicho,  walishtuka  kuona miili wa watu watatu, ikielea kwenye maji kisimani humo.
Askari Polisi kwa kushirikiana na wakazi  wa kijiji  hicho,  waliopoa miili yote lakini watoto  hao wawili  tayari walikuwa wamefariki, huku mama yao akiwa amekunywa maji  mengi  na kupoteza fahahamu.

Kutokana na hali hiyo,  wakazi  hao walipandwa na hasira  na kwenda kuvamia  nyumba  ya mtuhumiwa na kumkamata,  ili wamchome moto.
Hata hivyo, Kamanda  Kidavashari alisema  polisi walifanikiwa kufika kwa wakati  katika  eneo  hilo,  na kumwokoa  mtuhumiwa ambaye kwa  sasa  bado  ameshikiliwa Polisi  kwa  mahojiano.

Mama  wa watoto hao kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, alikimbizwa  katika Kituo  cha Afya  cha  Kijijini cha  ba  wilayani  humo,  ambako  amelazwa kwa  matibabu lakini  hadi jana bado alikuwa amezirai.
Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara  tu baada ya  uchunguzi  wa awali  wa shauri lake kukamilika.