Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa amesifia utawala wake kwa kuongoza taifa
bila ya kubaguana na amesikitishwa na matukio ya udini, ambayo
yanaashiria kuvuruga amani na utulivu wa Tanzania katika siku za
karibuni.
Akitoa salamu zake baada ya kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki
la Bukoba, Desdelius Rwoma, Mkapa alisema anachojivunia ni kuheshimiwa
na waumini wa madhehebu yote.
“Katika kipindi cha uongozi wangu, viongozi wa madhehebu yote walikuwa
wakinisisitizia kuwa sisi sote ni ndugu pamoja na tofauti zetu za
kiimani. Wakati wa utawala wangu nilijitahidi kwa uwezo wangu wote
kuwahudumia wananchi bila kuwepo kwa malalamiko ya kubaguana katika
jamii,” alisema Mkapa, ambaye aliiongoza Tanzania kuanzia mwaka
1995-2005.
Mkapa alionya kuwa taifa limeacha misingi aliyoiacha Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mara zote alisimamia umoja wa taifa.
“Wakati wa utawala wangu nilijitahidi kwa uwezo wangu wote kuwahudumia
wananchi bila kuwepo kwa malalamiko ya kubaguana katika jamii,” alisema.
Mkapa ambaye hakupanga kuongea lolote katika tukio hilo, alitaka taifa
lijenge utamaduni wa kupendana, huku akilaumu kuwa kizazi kipya cha
uongozi kimeanzisha mambo ya ajabu ya kukosa upendo na kudhalilishana.
Pia alitahadharisha kuwa zama hizi kumeibuka mitafaruku mbalimbali na
kuwakumbusha Watanzania kuwa ni wakati wa kumwabudu Mwenyezi Mungu.
Mkapa alisema mara nyingi alishauriana na viongozi wa dini katika
masuala ya kijamii na kiroho na kumtaja askofu mpya wa Bukoba, Rwoma na
Mtangulizi wake aliyestaafu Nestory Timanywa kuwa alishirikiana nao
katika masuala ya wananchi. Onyo la Mkapa limekuja siku chache baada ya
Rais Jakaya Kikwete kukemea mambo ya kidini na kutetea Serikali yake
haiongozi kwa misingi ya ubaguzi.
Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alikwenda mbali
zaidi na kudai amekuwa akilalamikiwa na viongozi wa madhehebu ya
Kikristo na yale ya Kiislamu.
Maneno ya Mkapa na Kikwete yamekuwa katika kipindi hiki taifa likiwa
limetikiswa na matukio yenye mwelekeo wa chuki za kidini. Matukio
makubwa yakiwa yale ya kuuawa wa Padri Evarist Mushi huko Zanzibar na
Mchungaji Mathayo Kachila wa Geita.
Pia kupigwa risasi kwa Padre Ambrose Mkenda na kumwagiwa tindikali kwa
Sheikh Fadhil Soraga na vurugu za mambo ya kuchinja huko Geita na
Tunduma.
Askofu Mpya wa Bukoba Rwoma alimshukuru Mkapa kwa kuzungumzia umuhimu wa
amani ya nchi, huku akisisitiza suala la upendo miongoni mwa wananchi.